January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wapata maji mwaka huu,toka nchi kupata uhuru mwaka 1961

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Muheza

WANANCHI wa vijiji vya Mbomole na Sakale, Kata ya Mbomole, Wilaya ya Muheza mkoani Tanga wameishukuru Serikali kwa kuwapatia maji ya bomba kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Kupitia Diwani wa Kata ya Mbomole Robert Zakharia, wananchi hao walikuwa hawajapata maji ya bomba tangu nchi kupata Uhuru mwaka 1961, wakati maji wanayokunywa wananchi wa Jiji la Tanga na maeneo mengine, moja ya chanzo chake ni Kata ya Mbomole.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba akiweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji Mbomole/Sakale uliopo Kata ya Mbomole wilayani Muheza

Ameyasema hayo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba, ambaye alifika Kijiji cha Mbomole ili kukagua na kuweka Jiwe la Msingi mradi wa Maji Mbomole/Sakale, ikiwa ni sehemu ya kutembelea miradi ya maji Wilaya za Pangani, Muheza na Mkinga.

“Tunaishukuru Serikali kwa kutupatia mradi wa maji,wananchi walikuwa hawana maji ya uhakika wakati chanzo cha mto Zigi kipo Kata ya Mbomole lakini waliokuwa wanafaidika na maji hayo ni wananchi wa Tanga na Muheza mjini,” amesema Zakharia.

Tenki la maji lenye ujazo wa lita 150,000 kwa ajili ya mradi wa maji Mbomole uliopo Kata ya Mbomole wilayani Muheza

Akitoa taarifa ya mradi kabla ya Mkuu wa Mkoa kuweka jiwe la msingi, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Muheza Mhandisi Cleophace Maharangata amesema mradi wa Maji Mbomole/Sakale unajengwa kwa gharama ya zaidi ya milioni 877.5na ulianza utekelezaji wake Julai 18, 2022, na unategemewa kukamilika Novemba 30, 2023.

Mhandisi Maharangata amesema mpaka sasa mradi umefikia asilimia 72 ya utekelezaji huku kiasi cha zaidi ya milioni 215.3 zimekwishatumika na Mkandarasi M/s Daska Investment Company Ltd kutoka Mugumu mkoani Mara anadai kiasi cha zaidi ya milioni 244.5.

“Mradi huu utakapokamilika utasaidia jamii katika upatikanaji wa maji safi na salama, kupungua kwa magonjwa yatokanayo na ukosefu wa maji safi, na kuchochea ukuaji wa uchumi wa vijiji vya Sakale na Mbomole” amesema Mhandisi Maharangata.

Wananchi wa Kata ya Mbomole, wilayani Muheza wakiwa kwenye mkutano wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba, ambapo alizungumza na wananchi hao mara baada ya kuweka jiwe la msingi mradi wa maji Mbomole/Sakale

Maharangata amesema mradi huo umechelewa kutokana na changamoto ikiwemo kukauka kwa chanzo cha maji na kufanya kusimama kwa utekelezaji wa mradi na kutafuta chanzo kingine, kuwepo kwa mvua kubwa inayoendelea kunyesha na kupunguza kasi ya utekelezaji wa mradi, na kuchelewa kwa upatikanaji wa fedha za kumlipa mkandarasi.

“Pamoja na changamoto zilizojitokeza, tunaishukuru Serikali kwa kutupatia fedha za utekelezaji wa mradi huu wa maji, na utakapokamilika unatarajia kuhudumia vijiji vya Sakale na Mbomole vyenye jumla ya wakazi 3,715,” amesema Maharangata.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Muheza Mhandisi Cleophace Maharangata (katikati) akimuonesha ramani ya Mradi wa Maji Mbomole/Sakale, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba (kulia).