Na Hadija Bagasha,TimesMajira Online, Tanga
Zoezi la upimaji wa viwanja Katika eneo la Lusanga wilayani Muheza Mkoani Tanga limeingia dosari baada ya wananchi wa maeneo hayo kupinga mchakato huo huku wakimuomba Rais kuingilia kati jambo hilo.
Wananchi hao wamesema wanao umiliki na maeneo hayo kiasili lakini kinachowashangaza ni kuona mpango wa upimaji ambao wamedai haukuwashirikisha na kufikia maamuzi ya pamoja.
Jumbe Mwatamwa Saasita amesema kuwa mpango huo unalenga kuwadhulumu maeneo yao ambayo wameyarithi kutoka enzi za mababu na kuyatunza kama maeneo yao ambayo wamekuwa wakijipatia kipato kwenye kilimo cha machungwa.
Alisema kwa mujibu wa maelezo ya mpango huo eneo lako likipimwa likakutwa na viwanja 10 mmiliki wa asili anapewa viwanja vitatu jambo ambalo wanaliona kama ni jambo ambalo litawaathiri kiuchumi.
“Haya ni maeneo yetu ya asili ya kudumu na ndio tunayoyategemea kwajili ya kusomesha watoto wetu tunategemea sisi kwa kila kitu maeneo haya lakini tunashangaa sana kuona hawa watu wanasema wametumwa na baadhi ya viongozi, “alisisitiza.
Kwa upande wake Omary Abdul Mkazi wa Lusanga A amesema anasikitika sana kuona mashamba yao yakipokonywa na kumuomba Rais kuingilia kati jambo hilo kabla mpango huo haujafanyika na kuhatarisha hali ya amani.
Alisema kupitia maeneo yao watoto wao wanasoma vyuo vikuu nasekondari na ndio mahali makazi yao yalipo na kwamba watu hao wamekuja kwa kisingizio cha kupata ruhusa kutoka kwa viongozi wa juu huku wakitishia maafa.
Naye Iligeni Hamisi Shekue amesema kuwa maeneo yanayotakiwa kugawiwa ni maeneo ambayo yana michungwa ambayo ndio muhimili wa familia zao lakini wanashangaa jambo hilo kufanyanwa huku mwenyekiti akiandika mihutasari ambayo wanaikataa ya kuonyesha kwamba waliridhia mpango huo uendelee.
Akizungumzia malalamiko hayo Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Muheza Nassib Mmbaga alisema kuwa suala hilo la upimaji wa ardhi ni shirikishi na hakuna mtu aliyelazimishwa kupima na kueleza kuwa kila kipande cha ardhi katika nchi ni lazima kipimwe.
“Kitu ambacho hatutotaka ni ujenzi holela tumesema ili kuzuia ujenzi holela tuwasaidie wananchi kupunguza gharama za upimaji kwasababu nighali nikawatuma watu wakae na nyinyi wananchi wa Lusanga tujaribu kutengeneza upimaji shirikishi ambao utawapunguzia gharama waliopo tayari wafanye na ambao hawapo tayari wasubiri kulipia gharama za upimaji muda ukifika, “amesisitiza Mkurugenzi Mmbaga.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best