Na George Mwigulu,Timesmajiraonline
,Mpanda.
TAKRIBANI Wananchi 500 wakazi wa Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi wametishia kuzuia ujenzi wa mradi wa maji wa miji 28 wenye thamani ya fedha zaidi bil.22 unaotekelezwa kupitia chanzo cha maji cha bwawa la Milala.
Mkazi wa mtaa wa Shanwe, Helena Magwaya amenukuliwa akisema “ tumeondoka kwenye makazi yetu na nyumba kubomoa kwa ahadi ya kupewa fidia ya fedha lakini ni miaka miwili tumeishi pasipo malipo”
Huyo ni mmoja wa wakazi wa manispaa ya Mpanda akizungumza na wanahabari Octoba 19, 2024 katika mtaa wa Shanwe baada ya wananchi kujitokeza kushinikiza kulipwa fedha za fidia za kupisha ujenzi wa mradi huo.
Ujenzi wa mradi wa maji wa miji 28 ni kati ya miradi inayotekelezwa nchini kwa ajili ya kuondoa tatizo la uhaba wa maji safi na salama ambapo wananchi wa mitaa ya Shanwe,Kigamboni na Mtemibeda Manispaa ya Mpanda wanaipongeza serikali lakini hawako tayari kupitia mradi huo kuishi maisha magumu.
Mwenyekiti wa wahanga wa madai hayo, Peter Matyampula ameeleza mnamo mwaka 2017 serikali kupitia mamlaka za uhifadhi wa bonde walifika katika meneo yao na kuwataka kupisha chanzo cha bwawa Milala lakini haikuwezekana kutokana na mkurugenzi tayari alikuwa ameshawauzia wananchi viwanja ndani ya mita 300 na kujenga nyumba za makazi.
“ Hata ilipofika kamati ya mawaziri nane mwaka 2022 tuliwaeleza kwamba hatujavamia eneo hili kwa sababu bwawa hili nila kutengeneza…walituelewa nasi tukaiomba serikali kutulipa fidia” Amesema Mwenyekiti huyo.
Amesema “Mwaka 2022 Mkuu wa Mkoa alikuja kutoa marufu ya kutokuendelea na shughuli yoyote kwenye maeneo yetu hadi pale serikali itakapotoa maelekezo mengine”
Matyampula amefafanua baada ya kukaa kwa muda mrefu bila malipo waliandika barua kwenda kwa Mkuu wa Mkoa na kwa nakala kwenda kwa Rais na waziri mkuu ndipo baada ya siku saba Mkuu wa wilaya ya Mpanda na Katibu tawala walifika kuongea na wananchi.
“DC alisema kaeni mkao wa kula maana muda ni huu umefika tunaomba ili shughuli ifanyike sasa kitu kinachotakiwa kufanya ni uthamini…nasi wananchi tulikubali.Ni kweli walikuja wathamini na wakasema hela zenu zipo lakini jambo la kushangaza hatujalipwa chochote” Amesema Matyampula.
Amesema “Hatuna mahali pakwenda, ukienda barabara ya Tabora utaambiwa kuna mashamba ya watu, ukienda Mishamo utaambiwa kule kuna makazi ukienda barabara ya sumbawanga utaambiwa kuna hifadhi”
Matyampula ameeleza kuwa mradi tayari umeanza kujengwa na kufanya hivyo ni kinyume cha sheria mbayo inasema uthamini unapofanyika ndani ya mienzi 6 wananchi walipwe fidia yao. Taasisi yoyote inapochukua ardhi ya mwananchi iwe tayari imetenga fedha za kuwalipa.
Ameongeza “wananchi kwa sasa wanaishi kwenye nyumba za kupanga na wala hawamudu gharama za pango,maisha yetu ni magumu,mfano mimi mwenyewe nilikubali uthamini wa Mil 1.2 kwa hekari moja ambapo ningeweza kuuza kwa watu wengine ningeweza kuuza kwa Mil 4 kwa hekari nani hekari 10 tizama faida hiyo.
John Kuchela amesema kuwa hawako tayari kuona suala la malipo ya fedha zao za fidia litumike kisiasa kwani hadi sasa wametumia juhudi kubwa ili walipwe imeshindikana.
Kuchela amesema wameweza kuwasiliana na Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini na viongozi wengine kutafuta msaada lakini imeshidikana “ Uchanguzi utafika na kujifanya kama tatizo hili hawakulitengeneza wenyewe na kujifanya wenye huruma hatutakubali kuwa daraja la kisiasa”.
Kaimu Mkurugenzi wa Muwasa Mpanda Mkoa wa Katavi,CPA Rehema Nelson uthamini ulifanyika mwenzi wa tano kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha,Maji na watu wa ardhi wa Manispaa ya Mpanda.
“Walifanyiwa uthamini na kuhakikiwa madeni yao na kila mwananchi aliyefika eneo hilo na aliyekuwa akidai alifika kuhakiki na kusaini kwa ajili ya ulipwaji” Amesema Kaimu Mkurugenzi huyo.
CPA Rehema amesema taratibu zilizopo kwa sasa zipo Wizara ya Fedha na anaimani watalipwa hivyo akawaomba wananchi hao kuwa wavumilivu.
More Stories
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya