December 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi Lushoto watakiwa kulinda vyanzo vya maji

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto

WANANCHI wametakiwa kulinda vyanzo vya maji ili viweze kuwa endelevu na kurithisha rasilimali maji kwa vizazi vijavyo kwa maendeleo ya Taifa na dunia, kwani kuendelea kuharibu vyanzo hivyo vya maji ni kujiangamiza wanadamu wenyewe na viumbe vilivyopo kwenye uso wa dunia.

Hayo yamesemwa Disemba 19, 2024 na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Lushoto William Mwakilema wakati anafungua kikao cha tatu cha Jukwaa la Wadau wa Usimamizi wa Rasilimali za Maji Kidakio cha Mto Umba, kilichoandaliwa na Bodi ya Maji ya Bonde la Pangani, na kufanyika mjini Lushoto.

“Bodi ya Maji Bonde la Pangani imepewa jukumu na Serikali ambalo ni kusimamia vyanzo vya maji ili viweze kuwa endelevu ili viweze kutuhudumia sisi na vizazi vijavyo. Na hili ni jambo la muhimu, sababu wakati mwingine tunakuja kwanza kulaumu au kunyooshea kidole kwa kuwa sisi tumejivua jukumu. Kwa hiyo tushirikiane na hawa wenzetu kwa kazi kubwa wanayoifanya katika utunzaji wa vyanzo vya maji ili huduma ya upatikanaji wa maji iwe endelevu,”amesema Mwakilema.

Mwakilema amesema uwepo wa taasisi mbalimbali za masuala ya maji na mazingira kwenye kikao hicho inampa taswira kuwa upo ushirikiano mkubwa wa wadau katika kusimamia rasilimali maji, na kumpa matumaini kuwa kama wataendelea na ushirikiano huo, azma ya kulinda vyanzo vya maji itafanikiwa katika Mkoa wa Tanga.

Mwakilema amewatahadharisha baadhi ya wadau ambao ni watumia maji ikiwemo baadhi ya Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji (CBWSO’s) wilayani Lushoto ambao hawaombi vibali wala kulipa ada kwa matumizi kwa wenye mamlaka, Bodi ya Maji Bonde la Pangani kama sheria inavyowataka kufanya hivyo.

“Hivyo naelekeza CBWSO’s pamoja na wadau wengine kutimiza wajibu wenu kwa kuomba vibali kutoka Bodi ya Maji Bonde la Pangani, pamoja na kulipia ada ya matumizi ya maji ambalo ni takwa la kisheria. Pamoja na kwamba ni takwa la kisheria, na kama tunavyosema ili uendelevu uwepo, pia itatusaidia Bodi yetu kupata rasilimali fedha ili kuweza kuendeleza kazi zake,”amesema Mwakilema.

Mwakilema ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe,amewataka wadau waelewe kuwa uchumi na ustawi wa kazi katika kidakio cha Mto Umba na maeneo mengine ya Bonde la Pangani, inategemea sana, tena kwa kiwango kikubwa, usimamizi bora wa vyanzo vya maji, na wote waliopo maeneo hayo ni wanufaika wa maji, hivyo hawana budi kushiriki kikamilifu katika kulinda rasilimali hiyo ya maji kama inavyowekwa msisitizo na viongozi wa kitaifa.

Amesema anafahamu kuwa, pamoja na mabadiliko ya tabianchi na kupungua kwa wingi wa maji, anafahamu jitihada zinazofanywa na Bodi ya Maji Bonde la Pangani la kuweka mipaka (vigingi) na kutunza mazingira kwa kupanda miti kwenye vyanzo vya maji, kuweka mabango na kutoa elimu ya utunzaji mazingira, ili kuweka uhai Bonde la Pangani kuwa endelevu katika upatikanaji maji wakati wote.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Lushoto Ali Daffa anashangazwa na taasisi za Serikali kukinzana, kwani wakati Bodi ya Maji Bonde la Pangani inafanya jitihada kutunza mazingira kwa ajili ya upatikanaji maji, Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) yeye anapanda miti ambayo ni hatari kwa uhifadhi wa maji, hivyo kutaka kuliweka sawa jambo hilo ili lisiweze kuleta athari kwa wananchi huko baadae.

Mbunge wa Jimbo la Lushoto Shaaban Shekilindi maarufu kama Bosnia,amesema suala la maji linaweza kusababisha Vita ya Tatu ya Dunia kama litafanyiwa mchezo mchezo kwa watu kuharibu vyanzo vya maji, huku akiwataka wananchi waweze kusaidia kulinda vyanzo vya maji ikiwemo viongozi wa vijiji kuwa walinzi wa vyanzo hivyo.

Shekilindi pia amewataka watu wenye vyanzo mbalimbali vya maji wasinyang’anywe, na badala yake wapewe ushirikiano ili waweze kuhudumia wananchi, kwani kama Serikali ingeweza kufikisha maji kwenye eneo husika, hakuna mwananchi angeweza kuhangaika kuchimba visima  ama kuweka mabomba msituni, ukiona hivyo, hilo eneo bado Serikali haijapeleka maji ya kutosha.

Awali, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani Mhandisi Segule Segule amesema maji ni rasilimali za nchi kama ilivyo madini, ardhi na misitu, lakini haizungumziwi kama ilivyo rasilimali nyingine. Lakini akawaeleza wadau, maji ni rasilimali ambayo nayo inatakiwa kutunzwa kama ilivyo madini na ardhi ama misitu, na kama itaachwa na ikatoweka itaweza kuleta athari kubwa kwenye jamii.

“Bodi ya Maji Bonde la Pangani ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Maji. Imepewa majukumu ya kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali maji. Kama mnavyojua utaratibu wa nchini yetu, rasilimali za nchi  zipo chini ya Rais, na yeye amekasimu madaraka yake kwa wizara na taasisi mbalimbali. Tunazo rasilimali ambazo ni maarufu kwetu kama madini, ardhi na misitu, na sio rahisi watu kuona wanatafsiri kama maji ni rasilimali.

“Na wengi wanaona maji ni kitu Mungu amekitoa kwa kila mtu, lakini sio kama sehemu ya rasilimali. Lakini maji nayo ni rasilimali ambayo tukiiacha na tusipokuwa na namna sahihi ya kuisimamia tutafupisha au kuathiri uendelevu wake. Uendelevu tunamaanisha rasilimali hii itumike kwa sisi tuliopo kama ambavyo tumeikuta, lakini na wenzetu watakaokuja baada ya sisi waweze kuitumia. Na ili lengo liweze kutimia ni lazima kwa namna moja au nyingine tushiriki kuhakikisha tunaitumia kwa namna ambayo hatutaiathiri rasilimali yenyewe na vyanzo vinavyoitoa,”amesema Mhandisi Segule.