Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto
TIMU ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC),imepokewa kwa vilio na wananchi wa Kijiji cha Mbwei,Kata ya Mbwei,Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kutokana na baadhi ya wananchi kunyimwa haki zao za msingi.
Timu hiyo ambayo ilifika Aprili 10, 2025 kijijini hapo, ilikutana na wananchi kwa ajili ya kuwapa elimu na kutoa msaada wa kisheria,ndipo baadhi ya wananchi walipojitokeza na kuangua kilio kuwa wamedhulumiwa haki za kumiliki mali baada ya baadhi yao kufiwa na waume zao.
“Mimi nilikuwa mke wa tatu, lakini baada ya mume wetu kufariki, mali zilizogawiwa ni zile zilizokuwa kwangu, lakini mali zilizogawiwa kutoka kwa mke wa kwanza na wa pili ambazo zote zilikuwa za mume wetu, mimi sikupata. Hivyo naomba ninyi mliokuja mnisaidie na mimi kupata mgao wa mali nyingine” alisema Subira Baraza.

Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Barikiel Msaky ambaye ni sehemu ya timu ya MSLAC, alimsikiliza mama huyo kwa kuchukua taarifa zake, na kuahidi atazipeleka kwenye vyombo vya sheria ili Subira Baraza aweze kupata haki zake.
Msaky alisema, moja ya changamoto wanayokutana nayo watoto ama mke baada ya mume kufariki ni mgawanyo wa mali, na hiyo inatokana na mume kushindwa kuandika wosia, lakini kama mtu anaandika wosia, ni rahisi kila mtu kujua atapata nini kutoka wapi, na kuwaasa wanaume kuandika wosia ambao hao watakaowaacha wataishi kwa salama.

“Kuandika wosia sio kujitabiria kifo kama wengi wanavyodhani,bali ni kuifanya familia yako kuishi kwa amani mara baada ya wewe kupumzika. Lakini kama hukuandika wosia, utaiachia tabu familia yako, na iweze kushindwa kuishi kwa amani. Na mtu upoandika wosia, hakikisha unauweka sehemu salama, na sehemu hiyo inaweza kuwa mahakamani, benki au RITA” alisema Msaky

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mbwei Fatuma Mzee alisema ni kweli huyo mama Subira Baraza mume wake alifariki tangu mwaka 2020, na amekuwa akifanya jitihada za yeye na watoto wake wa kike watatu kugaiwa mali bila mafanikio, lakini anaamini kwa timu ya MSLAC, huyo mama atapata haki yake.
“Ni kweli huyu mama alikutwa na changamoto ya kutopata mali za mume wake zilizokuwa kwa mke wa kwanza na wa pili baada ya yeye kufariki mwaka 2020, lakini mali zilizokuwa kwenye mji wake ziligawiwa kwa wake wote watatu na watoto wote wa wake watatu. Lakini naamini kwa timu hii ya MSLAC itaweza kumsaidia na kupata ufumbuzi wa suala lake” alisema Mzee.


More Stories
TMA yawataka wananchi kuzifanyia kazi taarifa inazotoa
TPDC, ZPDC zaendelea kushirikiana uendelezaji sekta ya gesi nchini
Nachingwea waanza kuona manufaa vituo vya kudhibiti wanyamapori waharibifu