Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe
Wananchi wa Kata ya Kalalani, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wataondokana na shida ya maji baada ya Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuwapelekea mradi wa maji ya bomba.
Hayo yalisemwa na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe Mhandisi William Tupa wakati wa utiaji saini wa mkataba wa mradi wa maji Kalalani mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo William Mwakilema na Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo, uliofanyika kwenye kata hiyo.
Mhandisi Tupa amesema, Kata ya Kalalani ni miongoni mwa kata 29 zilizopo Halmashauri ya Wilaya Korogwe ambayo inaundwa na vijiji viwili vya Kalalani na Mtoni Bombo vinavyokadiriwa kuwa na watu 3,762.
“Kwa kipindi kirefu huenda tangu kuundwa kijiji hiki, wananchi wamekuwa wakipata shida ya maji kwani maji yaliyopo kwenye visima yana chumvi na wakati mwingine maji ya Mto Umba unaopita pembezoni mwa kijiji hiki sio safi na salama hali hii inawafanya kuhangaika kutafuta maji Wilaya ya jirani ya Mkinga,”amesema Mhandisi Tupa.
Amesema pamoja na jitihada za Serikali za kutatua shida ya maji kwa kuchimba visima vifupi bado changamoto imeendelea kuwepo kwani uhitaji wa maji ni mkubwa.
“Serikali yetu kupitia taasisi yake ya RUWASA kwa kuzingatia ibara ya 100 ukurasa wa 149 ya Ilani ya CCM ya mwaka 2020 inayotaka huduma ya maji ifike asilimia 85 ifikapo mwaka 2025, hivyo imekamilisha taratibu zote za usanifu na manunuzi ya Mkandarasi wa kujenga Mradi wa Maji Kalalani,” amesema Mhandisi Tupa.
Mhandisi Tupa amesema wamekutana hapo kwa lengo la kusaini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji Kalalani na Mkandarasi M/s Bezalel Construction Company Ltd wa Dar es Salaam kwa mkataba wenye Na. AE-102/2022-2023/TAG/W/15.
Amesema lengo la mradi huo ni kutoa huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kwa wananchi wapatao 3,762 wa vijiji vya Kalalani na Mtoni Bombo.
Ambapo gharama za ujenzi wa mradi huo ni zaidi ya bilioni 1.6 ikiwa imetolewa asilimia 18 ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT Exemption) kupitia fedha za Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF)Na kazi zilizopangwa kufanyika kwa mujibu wa mkataba ni ujenzi wa banio (1 Intake),
kuchimba mtaro, kulaza bomba na kufukia urefu wa mita 40,818, ujenzi wa tangi lenye ujazo wa lita 100,000, ujenzi wa tangi lenye ujazo wa lita 50,000,
ujenzi wa vilula 17 vya kutekea maji, ujenzi wa BPT 1, ujenzi wa alama za bomba 420 (Marker posts), na ujenzi wa valvu chemba 20.
Mhandisi Tupa amesema kwa mujibu wa mkataba mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 12 unatarajiwa kuanza baada ya kukamilisha taratibu za kuondoa ongezeko la thamani ambalo ni asilimia 18 ya gharama ya mradi (VAT Exemption).
Amesema moja ya mafanikio ya mradi huo, ni pamoja na kuwapatia huduma ya maji wananchi wapatao 3,762, pia mradi huo utasaidia kutoa ajira kwa wananchi kipindi cha ujenzi na wakati wa uendeshaji.
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe,William Mwakilema amesema wananchi watanufaika na mradi huo, lakini ili mradi huo kuwa endelevu, ni lazima wananchi walinde miundombinu. Na pia kumtaka mkandarasi kutoa ajira za muda (vibarua) kwa kutoa kipaumbele kwa wananchi wa kata hiyo.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi