Na Joyce Kasiki,Dodoma
SERIKALI inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuwawezesha wananchi wa Bukoba na Mkoa wa Kagera kwa ujumla kushiriki katika ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba, kupitia mikopo yenye masharti nafuu.
Kauli hiyo ilitolewa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Ng’wasi Kamani wakati akijibu swali la Mbunge wa Bukoba Vijijini, Dkt. Jasson Samson Rweikiza.
Katika swali lake Dkt.Rweikiza alitaka kujua lini wananchi wa Bukoba watawezeshwa kupewa vizimba vingi zaidi vya samaki ili kukuza uchumi wao.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri huyo alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) tayari imetekeleza awamu ya kwanza ya utoaji wa mikopo ya vizimba, vifaranga pamoja na chakula cha samaki.
Amesema katika awamu hiyo, jumla ya vizimba 44 vyenye thamani ya shilingi milioni 986.8 vilitolewa mkoani Kagera, ambapo Bukoba ilinufaika na vizimba 30, Muleba 12 na Misenyi viwili huku wanufaika wakiwa ni wananchi 101.
Aidha, amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, Wizara imepokea shilingi bilioni 7 kutoka Hazina kwa ajili ya kuwawezesha vijana kupata mitaji kupitia mikopo yenye masharti nafuu.
Amesema,Fedha hizo zitalenga vijana 308 waliohitimu mafunzo maalum, wakiwemo vijana 32 kutoka Mkoa wa Kagera.
Katika hatua nyingine, Kamani alibainisha kuwa Wizara inatarajia kupokea sehemu ya shilingi bilioni 200, ikiwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais itakayotekelezwa ndani ya siku 100, fedha ambazo zitaelekezwa zaidi kwenye uwezeshaji wa mikopo ya vizimba vya samaki.
Amesema ,Serikali pia inaendelea kutafuta vyanzo vingine vya fedha ili kuongeza idadi ya wanufaika, hususan vijana wa Bukoba.
Aidha ametoa wito kwa Halmashauri zote zenye mazingira yanayofaa kwa ufugaji wa samaki kwa vizimba, kuelekeza sehemu ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa wananchi kwenye shughuli hiyo, ili kuongeza ajira na kukuza uchumi wa wananchi.

More Stories
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria