Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Wananchi wa Buhongwa, wilayani Nyamagana, mkoani Mwanza, wameeleza kuridhishwa na jitihada za serikali katika kutatua changamoto ya maji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA).
Septemba 8,2024, Waziri wa Maji,Jumaa Aweso, alitoa maagizo kwa MWAUWASA kufanya kazi usiku na mchana,alitembelea Kata ya Buhongwa na Lwahima. Katika kituo cha kusukuma maji cha Sahwa.Ambapo aliweka kambi katika eneo hilo na kushuhudia mafundi wakifanya kazi ya ulazaji wa bomba la inchi 12 lenye urefu wa kilomita 4.5 kutoka tenki la maji Sahwa hadi Buhongwa Center.
Jitihada hizo zilizaa matunda majira ya saa tano na nusu usiku, ambapo Waziri Aweso aliwasha mtambo wa kusukuma maji, na baadhi ya wananchi walishuhudia maji yakianza kutiririka katika maunganisho ya Buhongwa Center.
Septemba 11,2024,Mwenyekiti wa Mtaa wa Ng’ashi, Thomas Simon, aliongoza wananchi kutoa shukrani kwa serikali.Mara baada ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Agness Meena,kutembelea na kukagua mradi wa Matokeo ya Haraka,unaotekelezwa na MWAUWASA,kuona ufanisi wake na kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wa maeneo hayo ikiwemo Kata ya Lwahima na Buhongwa ambao wanakabiliwa na changamoto ya maji.
Mwenyekiti huyo wa mtaa,Simon, ameeleza kuwa,wakazi 7,000,wa maeneo hayo,walikuwa wakikabiliwa na adha ya ukosefu wa maji kwa muda mrefu, hasa katika maeneo ya AIC, Leonard Makoye, na John Lukanya. Maji yalikuwa yakipatikana mara moja kwa mwezi, hali iliyoleta usumbufu.
“Kiu ya wananchi wa Buhongwa ilikuwa maji, na mradi huu wa dharura tangu juzi umewapatia maji. Serikali inapaswa kusambaza miundombinu mipya ili maji yapatikane kwa urahisi zaidi ndani ya mita 60, kutoka bomba kubwa,”ameeleza Simon.
Stella Mkono, mkazi wa Buhongwa,ameeleza furaha yake, akisema, “Tulikuwa na changamoto ya ukosefu wa maji, lakini sasa tumepata faraja. Tunaishukuru Serikali kwa kutusikiliza na kutatua tatizo hili,” na kuongeza
“Bomba lilikuwa halitoi maji kwa muda mrefu,juzi nimeshangaa watoto kushangilia wakisema maji yanatoka baada ya kuona linatoa maji.Tunaishukuru Serikali kupitia MWAUWASA,Dk,kwa kutona wana Buhongwa na kukutua ndoo kichwani akina mama,”.
Joyce Abel aliongeza,“Sasa hatuhitaji kuamka usiku kutafuta maji. Tunashukuru sana serikali kwa kutuletea mradi huu wa maji, ambao umetuondolea adha hiyo,”.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Buhongwa, Dk. Lightness Masito, aliipongeza serikali kwa jitihada zake.“Kituo chetu kilikuwa kikikabiliwa na changamoto ya maji. Tulilazimika kuagiza maji kwa boza kwa matumizi ya usafi. Sasa tunapata maji kwa wakati na kwa kiwango cha kuridhisha,”.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Agness Meena, ameeleza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa mwaka mzima. “Tunafanya tathmini ya miradi ya maji ili kuhakikisha huduma inawafikia wananchi,”.
Awali, Naibu Katibu Mkuu huyo alitembelea mradi wa kimkakati wa maji Butimba, uliogharimu bilioni 72, unaozalisha lita milioni 48 kwa siku, kujionea ufanisi wake.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA, Neli Msuya, ameeleza kuwa,maji yalikuwa tatizo kubwa katika Jiji la Mwanza na maeneo ya pembezoni, kama Buhongwa. “Tumekuja na mradi wa Matokeo ya Haraka na sasa tunafanya majaribio kwa siku tano kuangalia ufanisi wake,”amefafanua.
More Stories
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa
Vikundi Ileje vyakabidhiwa mikopo ya asilimia 10, DC Mgomi avipa somo