Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline, Manyara
WANANCHI wa Kata ya Babati wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa madaraja saba pamoja na kufungua barabara katika kata hiyo ambapo kwa kipindi kirefu wamekuwa wakipata adha ya usafiri hususan kipindi cha mvua.
Akitoa pongeze hizo Diwani wa Kata ya Babati, Haruni Msalu, alisema kwamba wanamshukuru Rais kwa kuwatendea haki Kata ya Babati kwani Kata hiyo ilikuwa na makorongo mengi sana na kusababisha wananchi kuteseka hasa kipindi cha mvua na hivyo kusababisha kusimamisha kwa muda shughuli zao za kila siku.
Alisema katika kipindi cha Awamu ya sita Serikali kupitia TARURA imeweza kujenga madaraja yapatayo saba katika Kata ya babati katika eneo la Amboni C, Kambi ya Fisi, Hostel ya chuo cha uhasibu na Old Majengo-Angoni.
“Old Majengo kuja Angoni kulikuwa na korongo kubwa ambalo lilikuwa likipitisha maji kwenda ziwani, wananchi wakiwemo wanafunzi walikuwa wakipata tabu sana na hivyo kuathiri utendaji kazi kwa wanafunzi na wafanyakazi kwani iliwapasa kusitisha kwa muda kupita katika makorongo hayo”.
Msalu aliongeza kusema kuwa katika mpango wa TARURA wilaya ya Babati walitenga fedha kwaajili ya kujenga madaraja pamoja na kufungua barabara “kwakweli niwapongeze wafanyakazi wa TARURA kwa kutufungulia barabara kwani wananchi wa Babati njiji, majengo, Kware na mtaa wa Angoni wananufaika na ujenzi huu,” alisema.
“Kwa bajeti hii ya 2024/2025 tumeendelea kutatua changamoto ambapo daraja la mnara-Kijiweni sasa hivi ujenzi unakamilika na watu wameanza kupita lakini kazi ya kumwaga changarawe itaanza, niendelee kuwapongeza TARURA kwani katika pindi cha miaka minne kwa kujenga madaraja saba ni kazi kubwa sana na bado wanaendelea kutusikiliza na wananchi tupo na imani na Serikali” alisisitiza.
Hata hivyo diwani huyo amesema wao kama viongozi kwenye kata wanaendelea kusimamia miradi kwa kushirkiana na wataalam ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma zinazostahili.
Naye, Omary Nyange, Mkazi wa Mrara amesema wanatoa shukrani nyingi sana kwa Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa madaraja kwa kumalizika Wilaya ya Babati inapokea mazao mengi kutoka vijijini na biashara za mazao zinafanyika kwa wingi hivyo kukamilika kwa madaraja hivi sasa hakuna changamoto yeyote na malighafi zinaweza kufika mjini bila shida yeyote.
Aliongeza kwamba kwa kukamilika kwa madaraja hayo hivi sasa wanafunzi wanaweza kupata vipindi vyote vya masoko kwani hakutakuwa na kizuizi chochote katika makorongo hayo katika kata.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Mkazi wa Mrara Bw. Hamis Rajabu amesema Ilani yao imetekelezeka vizuri.
“Kwani ujenzi wa madaraja hayo ambayo yalikuwa ni kiunganishi kati ya babati mjini na vijijini, kero zote zimekwishwa hususan wale waendesha vyombo vya moto watakuwa wamepata mkombozi,”.
“Poa itatusaidia kutunyanyua kiuchumi kwani hakutakuwa na kitu kitakachowazuia tusiendelee na kusafirisha mazao husuan kipindi cha mvua,” amesema.
Pia Kaimu Meneja wa TARURA wilaya ya Babati, Mhandisi Naftari Lyatuu amesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa madaraja makubwa mawili na madaraja matano madogo pamoja na barabara ya babati-Mtuka (Km. 6) na barabara ya Nakwa (Km. 6) ambazo zinaunganisha kata tatu ikiwemo vyuo vya veta, Uhasibu pamoja na hifadhi ya taifa ya Tarangire kupitia geti la Mamile imeweza kufungua huduma nyingi za kijamii pamoja na utalii kwani wakazi wengi wanaishi upande huo wa madaraja yalipojengwa na hivyo kuweza kuwaunganisha na makao makuu ya mji wa babati.
More Stories
Wenje:Tuwanadi wagombea bila kuchafuana
Mtoto darasa la tatu adaiwa kujinyonga kwa kukosa nguo ya sikukuu
Jeshi la Polisi Katavi laanika mafanikio 2024