November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi 4346 Mkoani Tanga kunufaika na mradi wa REA

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Jumla ya wananchi 4346 kutoka katika Maeneo 82 Mkoani Tanga wanatarajiwa kunufaika na mradi wa usambazaji wa umeme wa REA katika maeneo ya pembezoni mwa miji hapa Nchini.

Mradi huo ambao unagharimu jumla ya shilingi bilioni 76.9 utakaotekelezwa katika Mikoa 8 hapa Nchini ambapo kati ya fedha hizo shilingi bilioni 11.5 zitatumika kwa jili ya utekelezaji wa mradi huo Mkoani Tanga.

Kufuatia mradi huo Wakandarasi wamesisitizwa juu ya umuhimu wa kununua vifaa kutoka kwa kampuni za ndani ya nchi ili kuimarisha uchumi wa Tanzania huku baadhi yao wakitakiwa kuacha tabia ya kununua bidhaa nchi za nje bidhaa ambazo zinapatikana hapa nchini jambo ambalo linasaidia kuimarisha uchumi wa nchi nyingine.

Kaimu Mkuu wa Mkoa Tanga Hashim Mgandilwa ameyasema hayo wakati wa makabidhiano ya mkataba wa utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa umeme wa Rea katika maeneo ya pembezoni mwa miji kwa mkandarasi kutoka kampuni ya OK ELECTICAL & ELECTRONICS SERVICE.

Mgandilwa amesema kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya wakandarasi kununua bidhaa nchi za nje bidhaa ambazo zinapatikana hapa nchini jambo ambalo linasaidia kuimarisha uchumi wa nchi nyingine.

Aidha amesisitiza juu ya mkandarasi aliyepewa kazi, kuajiri wafanyakazi kutoka kwenye maeneo ambayo mradi huo unatekelezwa ili kusaidia kuajiri vijana katika kazi ambazo sio za kitaalamu.

“Serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hasan imedhamiria kukuza uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja kwa kuweka miradi mingi ikiwemo huu uwekaji wa miundombinu ya umeme katika jamii yetu hususani maeneo ya pembezoni mwa miji kwa kuzingatia ubora wa nishati, “alisema Mgandilwa.

“Ninaomba kuwataka wakandarasi kama tulivyosikia hapa mradi huu unatekelezwa Tanga tunatamani tuone vibarua wote au ajira izile ambazo haziitaji taaluma tunaomba na tunawataka vibarua hao watoke kwenye maeneo husika ya mradi unapotekelezwa kumekuwa na kasumba baadhi ya wakandarasi wanatembea na watu wanatoka nao huko kwenye maeneo walikotoka na kuacha vijana wengi waliopo kwenye maeneo husika, “alisistiza.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa nishati vijijini (REA) Hassan Said amesema mradi huo ni mradi maalumu utatekelezwa kwa muda wa miezi 18 na utawafikia zaidi ya wananchi 4346

“Hii ni miradi maalumu na huwa inafanyika kwa awamu tofauti mradi huu utagusa Mikoa 8 kwa maana ya Kagera, Geita, Tabora, Kigoma, Mbeya, Singida Lindi pamoja na Mkoa wa Tanga na jumla ya gharama zote za mradi ni shilingi bilioni 76.9 fedha za serikali kwa asilimia 100,”alisema Mkurugenzi Mkuu Rea.

Aidha amesema mradi huo hautokuwa na nyongeza ya muda kwani miezi hiyo 18 inamtosha mkandarasi hata kabla ya muda huo na kuwataka wahakikishe wanafanya kazi ndani ya muda wakiopewa na wakala huku wakala wakisema hawatarajii kuwe na malalamiko ya umeme kusambazwa na kuwataka wafanye kazi katika maeneo yalioanishwa kwenye mkataba.

“Hii miradi yote ya nishati dhamira ya serikali ni kuboresha maisha ya wananchi na kuwapunguzia adha ya kukosa nishati ya umeme hatutarajii nia njema hiyo baadae ije kugeuka na kuleta malalamiko kutoka kwa wananchi kwenda kwa serikali yao, “alisema Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya OK ELECTRICAL.

Mhandisi Mrisho Masoud ameahidi kwenda kuyatekeleza maagizo yote waliyopatiwa kwani mradi huo unatekelezwa kwa fedha za serikali ambao ni mradi maalumu na ni mradi wa kimkakati.

“Sisi tupo tayari kuutekeleza kwa ufanisi wa hali ya juu hivyo niwatoe hofu katika mradi huu, “alisisitiza Masoud.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha miradi kutoka kampuni hiyo Levocatus Mwankema amesema kama ambavyo wameelekezwa na Mkurugenzi mkuu wa Rea watazingatia maelekezo na maagizo yote huku wakiahidi kuukamilisha, mradi huo ndani ya miezi 18 kama ilivyopangwa.

“Kwa sasa hivi baada ya kusaini mkataba tumeshaanza mazoezi mengine na mazoezi yanayofuata ni usanifu manununuzi ya vifaa ujenzi na kwenda hatua ya mwishoni ukamilisha na kufunga mradi hivyo baada ya vifaa kufika saiti itatuchukua kiasi cha miezi 6, “alisema Mkuu huyo wa kitengo.