Judith Ferdinand,Timesmajira online,Dodoma
Imeelezwa kuwa zaidi ya wananchi 15,000 tayari wameingia kwenye mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji wa hali ya barabara na kutoa taarifa pamoja na changamoto mbalimbali wanazo kutana nazo wanapotumia barabara katika maeneo mbalimbali nchini.
Hayo yameelezwa na Kaimu Meneja Mfuko wa Barabara Mhandisi Rashid Kalimbaga wakati akiongea na waandishi wa habari viwanja vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.
Ambapo Bodi ya Mfuko wa Barabara ilipo weka kambi Bungeni hapo kwa ajili ya kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mfumo huo kwa Wabunge.
Mhandisi Kalimbaga ameeleza kuwa kwa upande wa taarifa tangu kuzinduliwa kwa mfumo huo Julai mwaka 2022 jijini Mwanza tayari wamepokea taarifa za hali ya barabara zaidi ya 15,000 kati ya hizo taarifa 9,300, ambazo ni sawa na asilimia 62 tayari zimefanyiwa kazi huku taarifa 5,700 sawa na asilimia 38 bado hazijafanyiwa kazi.
Ambapo ameeleza kuwa utaona kwamba ni mfumo ambao unafanyakazi, taarifa zinakuja na zinafanyiwa kazi na mwananchi ambae anatoa taarifa anapatiwa mrejesho kwa wakati. kulingana na tatizo aliloliripoti.
“Taarifa hizi zinahusu hasa hali ya barabara kwa mfano kumetokea dharura kalavati limezolewa na mafuriko ya mvua, barabara imekatika, uwepo wa shimo barabarani au samani za barabara zimeibiwa basi wananchi wanaweza kutoa taarifa ya hali hiyo kupitia simu za mkononi, na taarifa hiyo itafika moja kwa moja kwa wakala wa barabara husika na watachukua hatua na kuitolea mrejesho kwa mtoa taarifa,” Mhandisi Kalimbaga.
Mhandisi Kalimbaga amesema kuwa Bodi ya Mfuko wa Barabara imeamua kuweka kambi Bungeni hapo ili kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mfumo huo wa kielektroniki wa ufuatiliaji wa hali ya barabara kwa wabunge ili nao wakishauelewa wasaidie kutoa elimu kwa wananchi jimboni mwao.
Hali itakayosaidia kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa haraka watakaoufahamu na kuutumia mfumo huo na hivyo kuongeza ulinzi kwenye miundombinu ya mtandao wa barabara nchini.
Kwa upande wake Mhandisi Jacob Mukasa kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara amesema kuwa mfumo huo ni rahisi kutumika na kila mwananchi kwa kuwa unapatikana kupitia simu za mkononi kwa kupakua mfumo huo uitwao Barabara kupitia App Store au Play Store au kwa kubonyeza *152*00# kuchagua namba nne halafu tano na kisha kufuata maelekezo ya kutoa taarifa za hali ya barabara.
Bodi ya Mfuko wa Barabara iliunda mfumo huo kwa kutumia wataalamu wake wa ndani ili kuwashirikisha wananchi katika ufuatiliaji wa hali ya barabara na hivyo kuongeza ulinzi wa miundombinu ya barabara ambayo Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuijenga.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato