December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanakilolo mna Bahati, Kitumieni CBE Kuwaendeleza Watoto Wetu- Majaliwa

Na Georgina Misama, CBE

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Kilolo mkoani Iringa kujiandaa kutumia fursa za masomo zitakazotoa wataalam mbalimbali kutokana na kuanzishwa kwa Kampasi mpya ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) wilayani humo.

Mhe. Majaliwa alisema hayo leo Julai 08, 2024 katika hafla fupi ya kukabidhi hati ya kiwanja chenye ukubwa wa heka 50 kwa CBE iliyofanyika kijijini Mbigili, Wilaya Kilolo Mkoa wa Iringa katika eneo ambalo chuo hicho kitajengwa.

“Wanakilolo tumieni bahati hii kwa kuwapeleka watoto wetu shule, changamkieni elimu, Tanzania sasa tunazalisha mazao mengi, wataalamu wa masoko tutawapata hapa, namshukuru Mkurugenzi kwa kuamua kutoa eneo hili kwa ajili ya ujenzi wa Kampasi nyingine ya CBE, chuo hiki ni kikongwe chenye hadhi ya Chuo Kikuu,” alisema Mhe. Majaliwa.

Vilevile alitoa rai kwa uongozi wa CBE kwenda kuweka sawa mipango ya ujenzi ili kuanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa chuo hicho bila kuchelewa, lakini pia aliwataka wazazi wote nchini kuwalinda watoto wa shule hususan watoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao.

Naye, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe alisema kuanzishwa kwa Kampasi hiyo mpya kunatarijwa kuzalisha wataalamu watakaokwenda kuendesha Sekta ya Viwanda na Biashara nchini.

“Tunaamini kwa kuwa na elimu bora tutakuwa na uwezo wa kuendeleza viwanda vyetu na kuongeza ushindani katika masoko ya kitaifa na Kimataifa, aidha tutakikisha Kampasi hii inakuwa ya kiwango cha juu katika kutoa elimu yenye kuleta tija kiuchumi na kijamii,” alisema Mhe. Kigahe.