Na Godfrey Ismaely, TimesMajira Online
WANAVIJIJI wa viijiji vya Tambani wilayani Mkuranga na Nyamwimbe wilayani Kibiti Mkoa wa Pwani wamelishukuru Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) kwa kuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia kuboresha na kuwezesha upatikanaji wa huduma za maji safi na salama, elimu na huduma za afya endelevu.
Pongezi hizo wamezitoa kwa nyakati tofauti wilayani humo wakati shirika hilo likikabidhi miradi mbalimbali ambayo limekuwa likifadhili ili iweze kuwanufaisha wananchi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo maeneo inapopita miundombinu ya gesi asili.
Mwanakijiji wa Kijiji cha Tambani, Said Seif wakati akishuhudia ugawaji wa vitanda kwa ajili ya wanafunzi watakaolala bweni Shule ya Sekondari Tambani ambavyo vilitolewa na TPDC anasema, heshima wanayopata kutoka shirika hilo inazidi kuwapa hamasa ya kuendelea kuwa walinzi wakubwa wa miundombinu inayopitisha gesi asilia.
Naye Aisha Juma ambaye ni mwanakijiji wa Kijiji cha Nyamwimbe anasema, kuchimbiwa kisima cha maji safi na salama katika Zahanati ya Kijiji ni moja ya hatua kubwa ya maendeleo, kwani “TPDC imetutua sisi akina mama wa Nyamwimbe ndoo kichwani”. Sasa maji tunapata saa 24 tena mengi na ya uhakika,”anasema.
Kwa upande wa TPDC wanasema, wataendelea kusaidia jamii kwa kushirikiana na Serikali katika vipaumbele vyake vya maendeleo mchini ili kufikia malengo ya uchumi wa kati.
Meneja Mawasiliano TPDC, Marie Msellemu kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wakati wa kukabidhi misaada katika Wilaya ya Mkuranga na Kibiti mkoani Pwani anasema, shirika hilo limekuwa na utamaduni wa kurejesha kwa jamii sehemu ya mapato yao.
Meneja huyo akiwa katika Shule ya Sekondari Tambani wilayani Mkuranga walipotoa msaada wa vitanda 40 vyenye uwezo wa kulaza wanafunzi 80 vikiwa na thamani ya sh.milioni 14.4 anasema, wataendelea kushirikiana na wananchi pamoja na uongozi wa shule hiyo wakati wote kwa ajili ya maendeleo ya elimu.
Anasema, wanatambua changamoto ambazo wanafunzi wamekuwa wakizipata hasa kutembea umbali mrefu kwa watoto wa kike ndio maana hawakusita kutoa mchango huo kwa ajili ya bweni maalum la watoto wa kike.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mkuranga, Mhandisi Mshamu Munde amewapongeza TPDC kwa kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya kwa kuisaidia Serikali hasa katika wilaya hiyo huku akisisitiza kuwa wataendelea kuilinda miundombinu ya shirika muda wote.
Pia Mkurugenzi huyo anawataka viongozi wa shule,wananchi pamoja na wanafunzi kutunza vitanda hivyo na mabweni kwa ajili ya maendeleo yao na kushirikiana kutatua changamoto ndogondogo zinazojitokeza.
Wakati huo huo, Meneja Msellemu amekabidhi mradi wa maji katika Zahanati ya Kijiji cha Nyamwimbe kilichopo Kata ya Mlanzi Wilaya ya Kibiti Mkoa wa Pwani ambao umegharimu zaidi ya sh. milioni 21.71, fedha ambazo zilitolewa na shirika hilo.
Msellemu anasema, TPDC wanaendelea kushirikiana na Serikali hasa katika kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibiti, Milongo Sanga ameishukuru TPDC kwa msaada huo wa ujenzi wa mradi wa maji ambao alisema, utakuwa msaada mkubwa kwa wanakijiji hao.
Pia anasema, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa TPDC ili kuendelea kuwasaidia wananchi katika changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyamwimbe, Tito Manyama Msiba anasema, mradi huo wa maji katika zahanati hiyo utakuwa wa baraka zaidi kwa wanakijiji na wagonjwa wanaofika zahanati hapo.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Tambani, Mohamed Issa anasema,vitanda hivyo vimesaidia kufikia lengo kwa asilimia 95 kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi wa kike kulala bwenini shuleni hapo ili kujisomea kwa uhuru zaidi.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi