Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Arusha
WANAHISA wa Benki ya CRDB wanatarajiwa ‘kuvuna’ kiasi cha bilioni 130.6 kama gawio la hisa kwa mwaka 2024 iwapo Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 29 wa Wanahisa wa benki hiyo wataidhinisha gawio la sh. 50 kwa hisa moja badala ya ile sh. 45 ya mwaka jana.
Hayo yamesemwa Mei 16, 2024 na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Dkt. Ally Laay kwenye mkutano wa waandishi wa habari na benki hiyo uliofanyika jijini Arusha.
“Faida yetu baada ya kodi imeongezeka na kufika bilioni 422.8 mwaka 2023 kutoka bilioni 351.4 mwaka 2022, ikiwa ni ongezeko la asilimia 21.
Kutokana na mafanikio hayo Bodi ya Wakurugenzi imependekeza gawio la sh. 50 kwa kila hisa sawa na ongezeko la asilimia 11.11 kulinganisha na gawio la sh. 45 lililotolewa mwaka jana.
“Iwapo pendekezo hili litaidhinishwa, jumla ya gawio litakalolipwa kwa wanahisa wote mwaka huu litakua bilioni 130.6 sawa na asilimia 34 ya faida halisi iliyopatikana, ambalo litakuwa limeongezeka kutoka bilioni 117.5 zilizolipwa mwaka wa fedha 2022,”amesema Dkt. Laay.
Dkt. Laay amesema mkutano huo wa Mei 18, mwaka huu, umebeba kauli mbiu ya “Ustawi Pamoja”, na utafanyika wakiwa katika mwaka wa pili wa utekelezaji wa mkakati wao wa biashara wa mwaka 2023-2027 ambao wanajivunia kwa kusema kuwa katika kipindi kifupi cha utekelezaji wake wameshuhudia mafanikio makubwa sio tu kwa kampuni Mama ya Benki ya CRDB, bali pia kwa kampuni zake tanzu za CRDB Bank Burundi na ile ya CRDB Bank DRC ambayo haina muda mrefu sokoni,pamoja na CRDB Bank Foundation na CRDB Insurance.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela amesema benki hiyo inayomilikiwa kwa mfumo hisa, inatambua jukumu muhimu ambalo wanahisa wake wanalo katika kuimarisha utendaji na kuamua mustakabali wa sasa na baadae.
“Maoni yao yanatuwezesha kukabiliana na changamoto, kutumia fursa na kutoa ukuaji endelevu kila mara. Hii imetusaidia, kujenga msingi wa ustawi wa pamoja ambao juu yake tumeendelea kushuhudia mafanikio makubwa kwa benki yetu, Wanahisa ambao ndio wawekezaji wetu, pamoja na jamii yetu kupitia uwezeshaji na uwekezaji ambao umekuwa ukifanyika,”amesema Nsekela na kuongeza
“Kwa mwaka huu, wanahisa wetu watapata nafasi ya kufahamu mwelekeo wa mkakati wetu mpya wa biashara wa muda wa kati wa miaka mitano 2023- 2027 wenye kaulimbiu ya evolve kwa kiingereza yenye maana ya mabadiliko, ambao tulianza kutekeleza mwaka jana pamoja na kufahamu maeneo ya kipaumbele kwa mwaka wa pili wa utekelezaji wa mkakati huu,”.
Kauli mbiu ya Mkutano wa Wanahisa kwa mwaka huu ni Ustawi wa Pamoja ambayo inaenda sambamba ya dira ya benki inayoangazia kuboresha maisha na uchumi nchini kupitia bidhaa na huduma bunifu, pamoja na programu wezeshi kwa makundi mbalimbali katika jamii.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi