Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
WANAFUNZI waliohitimu katika shule ya msingi Gongoni katika halmashauri ya manispaa Tabora wametoa msaada wa baiskeli 2 za matairi 3 (wheel chairs) zenye thamani ya sh 660,000 ili kusaidia walimu wastaafu 2 wenye maradhi ya kupoza miguu.
Akikabidhi msaada huo shuleni hapo, Kiongozi wa Umoja wa Wanafunzi hao Joseph Manyanda Sengerema alisema wametoa msaada huo kama fadhira kwa walimu wao waliowafundisha shuleni hapo.
Alitaja walimu waliokabidhiwa msaada huo kuwa ni Mwalimu Omari Fakhi na Ruben Nzumbi ambao wana maradhi ya kupooza miguu na kila mmoja amepewa basikeli 1 ya kutembelea yenye thamani ya sh 330,000.
Alibainisha kuwa msaada huo ni sehemu ya malengo yao ya kurejesha shukrani kwa walimu waliowafundisha na kuwawezesha kufika hapo walipo kimaisha ambapo kila mmoja sasa ana kazi yake na wengine wanaishi nje ya nchi.
Alifafanua kuwa walimu hao waliwajengea msingi imara ambao umewafikisha hapo walipo kimaisha ndio maana wakaguswa kuanzisha umoja huo na kuchangishana kiasi hicho ili wafanye kitu kwa ajili ya shule yao na walimu wao.
Sengerema ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa ndani katika hamashauri ya Wilaya ya Geita, Mkoani Geita, alisema mbali na msaada huo pia wanajipanga kutoa msaada wa madawati, viti, meza na kuingiza umeme katika shuleni hiyo.
Alibainisha malengo ya umoja huo wa ‘Ex Gongoni Primary School Tabora’ kuwa ni kuunganisha wanafunzi wote waliosoma shuleni hapo, kuimarisha ushirikiano na jamii, kusaidiana, kushauriana na kutengeneza fursa za kiuchumi na kibiashara.
Mnufaika wa baiskeli hizo Mwalimu Omari Fakhi aliwashukuru wanafunzi wake na kuwaombea dua njema katika maisha yao na kazi zao, huku akitoa wito kwa wanafunzi wengine kuiga mfano huo ili wapate baraka za walimu wao.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Feddy Mwiga alisema kitendo kilichofanywa na wanafunzi hao ni matunda ya malezi mazuri waliyopata shuleni hapo na kuwaomba isiwe mwisho bali waendelee kujitoa kuisaidia shule yao.
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango