December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Mkoa wa tabora Aggrey Mwanri (kulia) akisisitiza jambo mara baada ya kupokea vifaa vya kujikinga na Corona jana kutoka kwa Mtendaji mkuu wa Baraza la Taifa la watu wanaoishi na VVU (NACOPHA) Deogratis Rutatwa (kushoto)

Wanafunzi watakaorudi shuleni na mimba kuchukukuliwa hatua

Na Allan Ntana, Tabora

MKUU wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanatulia nyumbani na hawajihusishi na vitendo vya ngono katika kipindi hiki ambacho Serikali imefunga shule zote na vyuo ili kuwaepusha na maambukizi ya virusi vya corona.

Alitoa onyo hilo jana katika mdahalo maalumu wa wadau wa maendeleo uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Afya Tabora.

Alisema baadhi ya wazazi na walezi wameacha watoto wao kuzurura ovyo mitaani badala ya kuwasaidia watulie nyumbani na kujisomea kinyume chake baadhi yao hujiingiza katika vitendo vya ngono na michezo mingine isiyofaa.

Mwanri alisisitiza kuwa janga hili likipita serikali itafungua shule zote na vyuo ili kuruhusu wanafunzi kuendelea na masomo yao, hivyo alionya kuwa mtoto wa kike yeyote atakayerudi shuleni na mimba atachukuliwa hatua yeye na wazazi wake.

“Shule zitakapofunguliwa kazi ya kwanza tutakayofanya ni kuwapima watoto wa kike wa shule zote, yeyote atakayekutwa na ujauzito atachukuliwa hatua yeye na mzazi au mlezi wake,” alisema.  

Alimtaka Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO) Dkt. Honoratha Rutatinisibwa kwa kushirikiana na Waganga Wakuu wa wilaya zote (DMO’s) kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa ipasavyo na mwanafunzi yeyote atakayekutwa na ujauzito hatua kali zichukuliwe haraka iwezekanavyo.

Aidha aliwataka viongozi wa vitongoji na Watendaji wote wa vijiji na kata kuelimisha wazazi na walezi ili wakae vizuri na watoto wao katika katika kipindi hiki ili kuwaepusha na maambukizi ya ugonjwa wa covid-19 na mimba za utotoni.

Awali Mratibu wa Wajasiriamali wa Mkoa wa Tabora, Asha Shaban Mwazembe aliwataka wazazi na walezi wa watoto wote katika mkoa huo kuwachunga watoto wao katika kipindi hiki cha mapumziko ya dharura kabla shule hazijafunguliwa.

Alibainisha kuwa baadhi ya wanafunzi wameachwa huru kiasi kwamba hata kusoma hawasomi badala yake wamekuwa wakizurura ovyo mitaani badala ya kukaa nyumbani na kujisomea.