Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.
MKURUGENZI wa Elimu ya juu,Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia,Dkt.Kened Hosea amewataka wanafunzi wa Vyuo vikuu nchini kuwa mabalozi wa elimu ya sensa ya watu na makazi kwa jamii ili kufanikisha zoezi hilo linalotarajiwa kufanyika 23,Agosti 2022.
Dkt.Hosea ametoa kauli Jijini Dodoma wakati akizungumza katika Kongamano la umuhimu wa sensa lilioandaliwa na Jumuiya ya Wanafunzi,Taasisi za Elimu ya juu Tanzania (TAHLISO)ambalo limewashirikisha Wanafunzi mbalimbali wa Vyuo vikuu vya Mkoa wa Dodoma.
“Vijana ni chachu ya maendeleo hivyo mnapaswa kutumia majukwaa mbalimbali kutangaza umuhimu wa sensa,nani anapaswa kuhesabiwa pamoja na taarifa zitakazo kusanywa wakati wa sensa ikiwa ni pamoja na kuhimiza wanajamii kuweka umuhimu wa kumbukumbu za watu wote waliolala katika kaya usiku wa kuamkia siku ya sensa,
“Nitoe rai kwa wanafunzi wote wa Vyuo vikuu nchini kuhakikisha mnatumia majukwaa mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii kuhakikisha watu wanatambua umuhimu wa kuhesabiwa na kuwa na utayari wa kuhesabiwa,tukifanya hivyo tutairahisishia Serikali kutimiza wajibu wake kwa wananchi kulingana na idadi ya watu ya eneo husika ikiwa kama msingi mkubwa wa ugawaji ya keki ya taifa kwa kila eneo la utawala hapa nchini,”amesema
Pamoja na hayo ametumia nafasi hiyo kuwaasa wanafunzi hao kutembelea mara kwa mara tovuti za Wizara ya elimu kujionea fursa mbalimbali za elimu ikiwemo nafasi za masomo ya nje ya nchi ,ajira na nyinginezo.
Kwa upande wake Kamisaa wa Sensa wa Tanzania bara Anne Makinda akizungumza katika kongamano hilo amesema sensa ya mwaka huu ni shirikishi kutokana na kufanyika kwa hamasa katika makundi yote huku akiwasisitiza vijana kuendelea kutoa Elimu kwa jamii kuhusiana na umuhimu wa zoezi hilo kwa Taifa ili watu wakubali kuhesabiwa, na kwa kufanya hivyo nchi ipate takwimu sahihi ambazo zitatumika katika maamuzi ya kimaendeleo katika nchi kwa miaka ijayo.
Amesema kwenye jamii ambazo wanatoka wafugaji wamezunguza na viongozi wao takribani mia sita kwa mwezi mmoja uliopita Mkoani Dodoma, na wameeleza namna watakavyo kwenda kufanyakazi ya kuwawaelimisha kuhusu umuhimu wa sensa ya watu na makazi katika maeneo hayo ya Ngorongoro na manyara.
“Ili kufanikisha zoezi la sensa ya watu na makazi kwa mwaka huu tumeamuwa kutumia vijana ambao wanatoka katika maeneo hayo kwa vile wanafamiana pamoja na kutambua maeneo kwa urahisi tofauti na yule ambaye anatoka eneo lingine,”amesema Makinda.
Makinda ambaye pia ni Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kuwa zoezi hilo limetoa fursa ya ajira kwa vijana kutokana na kutoa nafasi laki mbili za ukarani ili kufanikisha zoezi la Sensa.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja