December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi Mzumbe wazungumzia mazingira na tahadhari ya Corona

Na Mwandishi Wetu

Wanafunzi waliowasili Chuo Kikuu Mzumbe kuendelea na Muhula wa Pili wa masomo utakao anza tarehe 01 Juni 2020, wameridhishwa na hatua za maandalizi zilizochukuliwa na Chuo hicho kuwakinga na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya CORONA (COVID-19).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa mahojiano na waandishi wa habari waliofika chuoni hapo kukagua maandalizi ya maeneo watakayotumia wanafunzi kusomea, wanafunzi hao wamesema wamefurahishwa na mazingira waliyoyakuta, na hivyo kuwaondoa hofu waliyokuwa wamejijengea kabla ya kufika chuoni hapo.

 “Tahadhari kubwa imechukuliwa, ukifika getini lazima kwanza kupimwa joto la mwili, mbali na uwepo wa vifaa vya kunawa mikono kila sehemu, matangazo ya tahadhari; huku tukisisitizwa  kuvaa barakoa muda wote tunapokuwa kwenye mikusanyiko” amesema Aney Daniel Mwanafunzi wa Mwaka wa Kwanza wa Shahada ya Sayansi katika Maendeleo ya Watu

Naye Hassan Salim, mwanafunzi wa mwaka wa tatu masomo ya sayansi na ICT, amesema hana hofu tena na usalama wa afya yake akiwa chuoni hapo kwani maandalizi yaliyopo yanamuhakikishia usalama na kuwataka Wanafunzi wenzake kila mmoja kuchukua hatua katika ulinzi binafsi wa afya, na kwamba kwa kufanya hivyo Jamii nzima ya Chuo itakuwa salama na masomo yao yatakamilika kama ilivyokusudiwa.

“Naomba niwatoe hofu wanafunzi wenzangu; kwakweli mawazo niliyokuja nayo na nilichokikuta ni tofauti, niliamua  nije mapema nione kwanza hali, lakini kwakweli mazingira ni rafiki sana kwa sisi kusoma na endapo kila mmoja wetu atachukua tahadhari basi usalama ni mkubwa kwetu sote” ameeleza

Awali akizungumza na waandishi wa Habari waliofika chuoni hapo kujionea maandalizi ya mapokezi ya Wanafunzi, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Rose Joseph amesema Chuo kimezingatia miongozo yote iliyotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Wizara ya Afya na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, kwa kuhakikisha tahadhari zote zinachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuandaa kwa wingi vyombo vya maji tiririka, sabuni, vitakasa mikono, elimu pamoja na kuandaa timu ya wataalamu wa Afya, watakaotoa huduma kwenye Kituo chetu cha Afya.

“Pamoja na kuandaa vipeperushi, mabango, na maelekezo maalumu ambayo yataendelea kutolewa kwa wanafunzi mmoja mmoja kadiri wanavyowasili na wakati wa madarasa, chuo tumeunda timu maalumu ya kushughulikia janga la CORONA, ambayo itakuwa inafanya kazi saa 24 kukagua, kuboresha na kushughulikia changamoto zote zitakazojitokeza, ili kuhakikisha wanafunzi na watumishi wanakuwa salama, sambamba na kukagua hali na mienendo ya wanafunzi kila wakati  ili kudhibiti maambukizi.” Amesisitiza

Ameziomba Mamlaka zinazohusika na usimamizi wa vyombo vya usafiri wa umma kwa kipindi hiki ambacho wanafunzi wanasafiri kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kuelekeza Chuo, kuelekeza wasafirishaji kuchukua tahadhari zote za kuwakinga wasafiri na maambukizi, pamoja na kuwakumbusha Wanafunzi kuchukua tahadhari binafsi zinazozingatia kanuni na miongozo ya Afya katika kujikinga na maambuzi wakati wote wanapokuwa safarini. Aidha; amewahakikishia Wazazi na Walezi kutokuwa na hofu kuhusu usalama wa watoto wao kwakuwa tahadhari kubwa imechukuliwa katika kuhakikisha wanakuwa salama wakati wote wakiendelea na masomo.

“Tuna namba ya simu maalumu kwa ajili ya kutoa taarifa wakati wa dharura, hivyo wanafunzi wataweza kuzitumia iwapo watahisi kuwa na dalili zozote au kuwepo wahisiwa ambao watapelekwa katika kituo maalum kwa vipimo vya awali kabla ya hatua zingine za matibabu kuendelea kama ulivyo mwongozo wa Wizara ya Afya” amesisitiza

Baadhi ya wanafunzi wameshawasili chuoni hapo kuanza masomo huku usajili ukiendelea kwa wanafunzi wanaoendelea na Muhula wa Pili wa Masomo, ambao utaanza tarehe 01 Juni 2020.  Zaidi ya wanafunzi elfu kumi na moja (11,000) wanatazamiwa kuripoti kwa Kampasi zake zote (Morogoro, Mbeya na Dar-es- salaam) kuendelea na masomo kwa ngazi mbalimbali.