March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi 89 waliofanya udanganyifu na kuandika matusi wafutiwa matokeo

*Ni katika upimaji wa kitaifa wa darasa la nne na kidato cha pili

*Kati yao 49 wa darasa la nne,huku 40 wa kidato cha pili

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online-Dar

BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limefuta matokeo ya wanafunzi 89 waliohusika na udanganyifu na kuandika matusi katika skripti zao wakati wa upimaji wa kitaifa wa darasa la nne na kidato cha pili.

Hayo yamebainishwa jijini Dar-es-Salaam Januari 10, 2026 na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani, Profesa Said Mohamed, wakati akitagaza matokeo ya kitaifa ya darasa la nne na kidato cha pili iliyofanyika Oktoba na Novemba 2025.

Amesema wanafunzi 41 walifanya udaganyifu na nane waliandika matusi kwenye skripti zao katika upimaji wa kitaifa wa darasa la nne huku wanafunzi 29 walifanya udaganyifu na 11 waliandika matusi kwenye skripti zao katika upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili

“Hatua hii imechukuliwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5(2)(j) cha Sheria ya Baraza la Mitihani, Sura ya 107, kikisomwa pamoja na Kifungu cha 30(2)(b) cha Kanuni za Mitihani za mwaka 2016,” amesema Profesa Mohamed

Aidha amesema ufaulu wa darasa la nne umeongezeka kwa asilimia 2.67, ambapo jumla ya asilimia 88 ya wanafunzi wamefaulu.

Amesema jumla ya wanafunzi 1,583,686 waliosajiliwa kufanya upimaji wa kitaifa wa darasa la nne wakiwemo wasichana 818,673 sawa na asilimia 51.69 na wavulana 765,013 sawa na asilimia 48.31.

“Kati ya wanafunzi waliosajiliwa wanafunzi 1,490,337 walifanya upimaji wakiwemo wasichana 780,586 sawa na asilimia 95.35 na wavulana 709791 sawa na asilimia 92.78 huku wanafunzi 93,309 sawa na asilimia 5.89 hawa kufanya upimaji “amesema Profesa Mohamed.

Aidha amesema mahudhurio yalifikia asilimia 94 sawa na wanafunzi 1,490,377 kutoka shule za msingi 20,508 huku ufaulu wa darasa la nne, wasichana wamefaulu kwa asilimia 53 na wavulana kwa asilimia 47.

Hata hivyo ubora wa ufaulu wa upimaji wa darasa la nne Profesa Mohamed amesema umeongezeka kwa asilimia 1.63 ikilinganishwa na mwaka 2024.

Kwa upande wa kidato cha pili, jumla ya wanafunzi 898,718 walisajiliwa kufanya mtihani huo, wakiwemo wasichana 497,891 sawa na asilimia 55.48 na wavulana 400,827 sawa na asilimia 44.5.

Profesa Mohamed amesema kati yao, wanafunzi 811,575 sawa na asilimia 91.3 walifanya mtihani katika shule za sekondari 6,223, huku wanafunzi 77,689 sawa na asilimia 8.7 wakishindwa kufanya upimaji licha ya kuwa walisajiliwa.