Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Ukerewe
Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ilipangiwa wanafunzi 840 kwa ajili ya kujiunga na kidato cha tano mwaka wa masomo wa 2023 kati yao hadi kufikia Agosti 18,2023 jumla ya wanafunzi 270 wameisha ripoti shuleni na kuanza masomo.
Hayo yamebainishwa Agosti 18,mwaka huu wakati Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Hassan Bomboko alipotembelea na kukagua shule za sekondari Bukongo, Pius Msekwa na Ukerewe lengo likiwa ni kujionea zoezi la kupokea wanafunzi wa kidato cha tano kwa msimu wa masomo wa 2023.
Katika shule ya sekondari Ukerewe ilipangiwa jumla ya wanafunzi 484 ambapo shule hiyo ina uwezo wa kupokea wanafunzi 500 wa bweni hadi siku hiyo jumla ya wanafunzi 120 wameripoti na kuanza masomo.
Mkuu huyo wa Wilaya Bomboko akiwa shule ya Sekondari Bukongo, ameeleza kuwa wanafunzi waliopangwa na serikali kujiunga na shule hiyo kwa masomo ya kidato cha tano ni 249 hadi siku hiyo ni wanafunzi 80 ambao wamewasili shuleni kutoka mikoa mbalimbali nchini huku shule hiyo ina uwezo wa kupokea watoto wasio pungua 250.
Ameeleza kuwa katika shule ya sekondari Pius Msekwa jumla ya wanafunzi 107 walipangiwa na serikali kujiunga hapo hadi siku hiyo ni wanafunzi 70 ambao wameripoti shuleni hapo na wameanza masomo hata hivyo shule hiyo ina uwezo wakupokea watoto 150.
Hata hivyo Bomboko amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ambazo zimefanikiwa kutekeleza ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya elimu.
“Nimekagua shule zote za kidato cha tano wilayani hapa nimejiridhisha, miundombinu ipo safi kila shule ina mabweni ya kutosha ya kuwalaza wanafunzi wetu watakaofika kuanza masomo mwaka huu, madarasa yapo ya kutosha mazuri na ya Kisasa,viti na meza zipo za kutosha,vitanda vipo,walimu wa tahahusi zote wapo na tayari wameanza kutekeleza wajibu wao wa kufundisha,”amesema Bomboko.
Sanjari na hayo ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wazazi wote wenye wanafunzi waliopangiwa kujiunga na kidato cha tano katika Wilaya ya Ukerewe kuwawahisha wanafunzi ili waanze masomo yao haraka pasipo kupoteza muda.
“Ninawasisitiza wazazi wote walio na wanafunzi ambao wamepangiwa katika Wilaya ya Ukerewe wafike kuanza masomo yao haraka ili kuondoa utofauti wa uelewa katika ufundishaji na ujifunzaji darasani,hatusubili masomo yameshaanza na kila kitu kipo sawa kuhakikisha wanafunzi wanapokelewa na wanapata huduma zote za msingi ikiwepo lishe,”amesisitiza Bomboko.
More Stories
5 “best” Bitcoin Online slots games
Best Web based casinos Norway Your own #1 Norwegian Online casinos 2024
Prof. Mwakalila asisitiza uadilifu, uzalendo kwa wanafunzi wapya chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere