Na Mwandishi wetu, timesmajira
WANAFUNZI 110 wenye mahitaji maalumu wa Shule ya Sekondari ya Jangwani wapewa msaada wa vifaa vya usafi, ikiwa ni maadhimisho ya siku ya kunawa mikono duniani.
Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika shule ya sekondari ya Jangwani, jijini Dar es Salaam, leo Oktoba 12, 2023, Mtaalamu wa Miradi wa Shirika la WaterAid, Rebecca Stanley, amesema wamekabidhi vifaa mbalimbali ili kuimarisha afya kwa wanafunzi wenye changamoto shuleni hapo.
“Leo tunakabidhi mahitaji haya yenye thamani ya Sh. milioni sita kwa wanafunzi hawa wenye uhitaji maalumu kwa ajili ya kuwasaidia kwenye masuala ya usafi binafsi na wa mikono,” amesema na kuongeza.
“Wanawake, wasichana na watu walio katika makundi maalumu ni makundi ambayo tunayapa kipaumbele kikubwa sana katika kazi tunazozifanya.”
Akipokea vifaa hivyo, Ofisa Afya wa Manispaa ya Ilala, Reginald Mlay, ameishukuru WaterAid Tanzania kwa kujumuika na wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika maadhimisho hayo.
“Tunashukuru sana Shirika la WaterAid, mbele yetu leo tumepokea sabuni za kunawia mikono, sabuni za kusafishia choo, vifaa vya kuhifadhia sabuni, sabuni za kuogea, sabuni za kufulia pamoja na taulo za kike na ndoo za kunawia mikono, tunaamini mahitaji haya yatawasaidia sana wanafunzi hawa katika masuala mazima ya usafi,” amesema Mlay.
Siku ya kunawa mikono duniani huadhimishwa Oktoba 15 kila mwaka na mwaka huu inaongozwa na kaulimbiu ya ‘mikono safi inaweza kufikiwa.’
Shirika la WaterAid Tanzania linashiriki maadhimisho ya siku ya kunawa mikono miezi michache baada ya kuadhimisha miaka 40 ya utendaji kazi hapa nchini.
Dhima ya Shirika hilo la kimataifa ni kuhimiza upatikanaji wa maji safi na salama, vyoo bora na huduma za usafi, ili kuwaepusha wananchi na magonjwa yatokanayo na uhaba wa maji na uchafu.
WaterAid inafanya kazi katika nchi 28, ambapo nchi 18 zipo barani Afrika.
More Stories
Dkt. Kikwete aipongeza Zanzibar, azindua Kituo cha Afya Kizimkazi
Dk Mwinyi ameifungua Skuli Kisiwani Tumbatu yagharimu Sh. Bii 7
Kyobya: Watakaohusika kudhoofisha jitihada za Serikali,Pori la Akiba Kilombero kushughulikiwa