March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi 10 wapata ‘Ufadhili wa Samia’

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma

WANAFUNZI  10 wamepata ufadhili wa masomo ya Shahada ya Uzamili kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended (SSE DS/AI+), unaolenga fani za Sayansi ya Takwimu, Akili Unde (AI) na Sayansi Shirikishi.

Hayo yamesemwa leo Februari 25,2026 na Waziri wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda  wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Wanafunzi waliopata ufadhili huo   wametakiwa kuangalia majina yao kupitia tovuti ya Wizara, Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania pamoja na Taasisi ya Nelson Mandela ili kupata taarifa zaidi kuhusu taratibu za kujiunga na masomo hayo.

Amesema,wanafunzi hao watasoma katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, huku wengine 10 wakitarajiwa kujiunga na masomo hayo katika Indian Institute of Technology Madras Zanzibar Campus.

Kwa mujibu wa Prof. Mkenda Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza rasmi kutoa ufadhili huo ikiwa ni sehemu ya kuimarisha rasilimali watu katika sekta ya sayansi na teknolojia nchini.

Amesema Serikali imeamua kuwekeza katika masomo hayo kutokana na mahitaji makubwa ya wataalamu wa takwimu, akili unde na sayansi shirikishi.

Amebainisha kuwa jumla ya shilingi bilioni tano zimetengwa kugharamia utekelezaji wa mpango huo, na kutoa wito kwa wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi hizo kwa kuchangia ufadhili kupitia Samia Scholarship.