February 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanachama CCM Kata ya Rujewa wajitokeza kufanya usafi kituo cha afya

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

KUELEKEA maadhimisho ya  miaka 48,ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM)wanachama wa chama hicho wamejitokeza kufanya  usafi katika kituo kidogo  cha  afya kata ya  Rujewa wilayani Mbarali mkoani Mbeya ili kuweka mazingira salama ya kutolea huduma za afya kwa wananchi.

Akizungumza Februari 2,2025 wakati wa zoezi hilo la kufanya usafi mmoja wa wachama wa cha hicho mkazi wa mtaa wa Mbuyuni kata ya Rujewa,Rose Kinyaga amesema wanamuunga mkono Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kufanya usafi katika maeneo ya hospitali na vituo vya afya.

Kinyaga amesema kwamba Miaka 48 ya CCM hawawezi kumuacha nyuma Rais Samia kwani kwa wilaya ya Mbarali amefanya mengi ikiwemo afya,elimu na barabara.

“Hii siku kwetu ni maalum kabisa tumetoka wanawake kufanya usafi hapa Kituo kidogo cha afya Rujewa kwa maana ametujengea hospitali nzuri,watumishi bora “amesema Kinyaga

Anna Mgonzi ni katibu jumuiya ya umoja wa wanawake kata ya Rujewa amesema katika kuadhimisha miaka 48 ya kuzaliwa kwa CCM wanakwenda na Rais Samia kutokana na Kazi kubwa anazofaya ikiwemo kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa wilaya hiyo.

“Wanachama wa cha Mapinduzi tumejitokeza kuja kufanya usafi katika kituo kidogo cha afya kata ya  Rujewa,tumeona tuje tufanye usafi hapa ili kuweka mazingira safi na usalama wa  kituo chetu cha afya ambacho kimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi,”amesema

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi kata ya Rujewa
Karume Mungulu amesema  ameshukuru wanachama wa chama hicho kujitokeza kufanya usafi katika hicho cha afya  na kusema kwamba  CCM ndicho chama chenye dhamana na kuwa kwa wilaya ya Mbarali hakuna kura itakayopotea kwa Rais Samia.

Jeremiah Makao ni Diwani wa Kata ya Rujewa amesema kwamba wamefika katika kituo cha afya Rujewa ili kumuenzi Rais Dkt.Samia katika suala la utunzaji mazingira pia wameanza rasmi shughuli za miaka,48,ya kuzaliwa kwa CCM ambapo kiwilaya wataazimisha February 5,2025 

Makao amesema kuwa maadhimisho hayo walianza Januari 30,2025 ambapo jumuiya ya wanawake walianza usafi, jumuiya ya wazazi na umoja wa vijana walizindua mashina  pamoja na kutembelea miradi ya maendeleo yote ikiwa ni kusherekea miaka 48 ya kuzaliwa kwa chama hicho sambasamba na kumpongeza Rais Samia kwa kazi nzuri ya kuleta maendeleo katika Taifa hili.

Aidha Makao amewataka wanachama wa chama hicho kuendelea kushikamana ili waendelee kushika dola pamoja na kukijenga chama hicho  na kuwa na mshikamano wa pamoja.