March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanaanchi wahimizwa kutumia huduma ya miadi ya kuonana na madaktari Bingwa MOI

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online , Geita

WANANCHI wametakiwa kutumia huduma ya kuweka miadi ya kuonana na madaktari bingwa kwa njia ya mtandao ili kuepuka usumbufu wa foleni na msongamano mkubwa unaosababishwa na wagonjwa wanaotoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari 24 Septemba 2025 kwenye maonyesho ya nane ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita , Daktari Bingwa wa Mifupa kutoka Taasisi ya Mifupa, Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI), Dkt. Kenneth Mgidange, amesema kuwa mfumo wa kuweka miadi kwa njia ya mtandao ni suluhisho la kupunguza muda wa kusubiri huduma kwa wagonjwa.

“Tunaendelea kuwahimiza wananchi, hasa kutoka mikoa ya mbali nje ya mkoa wa Dar es Salaam , kutumia huduma ya miadi kabla ya kufika MOI,hii itasaidia kupunguza msongamano, kuwapa huduma bora kwa haraka, na kuwapunguzia gharama zisizo za lazima,” alisema Dkt. Mngidange.

“MOI ni miongoni mwa taasisi za kibingwa nchini zinazotoa huduma za hali ya juu ikiwemo upasuaji wa ubongo,Kuondoa uvimbe kupitia njia ya pua,upasuaji wa mgongo kwa kutumia matundu madogo,Matibabu ya magoti kwa kutumia teknolojia ya kisasa kupitia matundu na matibabu yanayotumia teknolojia ya kisasa ya akili unde (AI)

Dkt. Mgidange ameongeza kuwa MOI imeendelea kuboresha huduma zake kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kuhakikisha wananchi wote, hata walioko mikoani, wanapata huduma bora bila ya kulazimika kusubiri kwa muda mrefu.

Kuhusu ushiriki wao kwenye maonyesho yanayoendelea mkoani Geita, Dkt. Mgidange amesema zaidi ya wananchi 170 wamejitokeza kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu afya zao. Baadhi yao wameelekezwa kufanya vipimo kwenye hospitali za karibu kabla ya kupelekwa MOI kwa matibabu zaidi.

“Mwitikio umekuwa mzuri sana. Wananchi wana hamasa ya kutaka kufahamu hali zao za kiafya, na sisi kama MOI tutaendelea kuwafikia kupitia maonyesho kama haya na pia kuwahimiza kutumia njia ya mtandao kuweka miadi,” alisisitiza.