December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wambura asikitishwa na makundi CCM Nyakato

Na Daud Magesa, TimesMajira Online,Mwanza


MJUMBE wa Baraza la Wazazi CCM Mkoa wa Mwanza, Alfred Wambura (Trump) amesikitishwa na makundi na ubaguzi unaoendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM),Kata ya Nyakato, wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Wambura ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano wa kumpongeza Menyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Majengo,Kata ya Nyakato Desudedit Malunde (CCM),alionesha masikitiko hayo.

Amesema katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024,wapo wana CCM wengi waliomba kupendekezwa na chama ili wagombee nafasi hizo za uongozi katika mitaa yao lakini ni mmoja tu aliyepata nafasi ya kuwakilisha chama kila mtaa kwa nafasi ya Mwenyekiti.

“Tunagombana ndani lakini baada ya kuteuliwa mmoja tubadilika na kuwa kitu kimoja,hiyo ndiyo demokrasia ndani ya Chama Cha Mapinduzi.Hata mimi niliwahi kugombea nikashindwa,nilikubali matokeo na kumuunga mkono,sasa CCM Kata ya Nyakato hali ni tofauti,”amesema Wambura.

Amesema kuwa anafurahishwa na wananchi kwa kumchagua Malunde kwa kipindi cha tatu na kuonya,kamwe makundi ya uchaguzi yakiendekezwa yatakigharimu chama na kukwamisha maendeleo,wenye nia na dhamira ya kuendeleza makundi ilhali uchaguzi umekwisha wajitathmini kwa maslahi mapana ya CCM na maendeleo ya wananchi.

Mjumbe huyo wa Barazala Wazazi ameonya makundi yakiendekezwa yatasababisha mpasuko mkubwa ndani ya chama na kutoa mwanya kwa wapinzani, hivyo wenye makundi wayavunje kwani uchaguzi umekwisha na walioshindwa wajipange upya kwa uchaguzi ujao.

Akijibu risala ya Mtaa wa Majengo iliyosomwa na Veronica Mtiro, ikieleza changamoto ya ukosefu wa vifaa vya ujenzi wa ofisi ya serikali ya mtaa huo,vinavyogharimu milioni 25 Wambura ameahidi kutoa bando mbili za mabati na saruji mifuko 10.

Ujenzi huo wa ofisi ya mtaa,tayari ulishaanza kwa nguvu za wananchi ambapo Mbunge wa Ilemela, Dkt. Angelina Mabula,alichangia matofali yenye thamani ya zaidi ya milioni 1.

Naye Masatu Mukabe mmoja wa wazee wa Kata ya Nyakato,amesema licha ya ushirikiano anadhani bado kuna mgawanyiko na watakuwa wanajidanganya, wakigawanyika ndani ya CCM watatengeneza mpasuko mkubwa.

Ameshauri wenye makundi yaliyosigana sababu ya uchaguzi kuungana kwa maslahi ya CCM na maendeleo ya wananchi wa Majengo huku akimtaka mwenyekiti na wajumbe, kuwasikiliza wananchi na wanachama pamoja na kutatua kero zao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyakati Desudedit Malunde amewashukuru mabalozi kwa kazi kubwa na wananchi kwa imani yao kwa iliyowasukuma kumchagua kwa awamu ya tatu,kwamba hana cha kuwalipa zaidi ya maendeleo ambayo ni dira yake.