Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mwanza
Juhudi za kuwatafuta watu watano ambao hawajaonekana baada ya mtumbwi waliokuwa wanasafiria kuzama ndani ya Ziwa Victoria zinaendelea kufanyiwa na Jeeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na wananchi wa Kisiwa cha Yozu na Burihaeke wilayani Sengerema mkoani hapa.
Ambapo jumla ya watu 23 walikuwa wakisafiri katika mtumbwi huo kati yao watu 17 wameokolewa wakiwa hai na mtu mwingine jinsia ya kike amepatikana akiwa amefariki dunia aliyetambulika kwa jina la Khadija Rashidi Badru mwenye umri wa miaka 26, mkazi wa Mbugani.
Tukio hilo lilitokea Agosti 05,2024 majira ya 2:00 usiku katikati ya kisiwa cha Yozu na Ziragula wakati wakitokea kwenye sherehe ya mashabiki wa Yanga (Yanga day) iliyofanyika kisiwani Yozu wakielekea kitongoji cha Itabagumba baada ya mtumbwi wao kuingia maji na kuzama.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza (DCP) Wilbord Mtafungwa,amewapongeza wananchi wa maeneo hayo kwa jitihada walizoonesha na kufanikiwa kuwaokoa watu 17 wakiwa hai baada ya ajali hiyo kutokea.
Ambapo watu watano ambao hawajapatikana ni Masaka Angote (60), mkazi wa Burihaeke, Edward Kachelemi anayekadiriwa kuwa na miaka 46, mkazi wa Burihaeke, Mashauri Isha Bakari, anayekadiriwa kuwa na miaka 42, mkazi wa Burihaeke, Jonathan Mutasyoba, anayekadiriwa kuwa na miaka 50, mkazi wa Kanyara na Shija Basikeli, anakadiriwa kuwa na miaka 30 na mkazi wa Yozu.
Mutafungwa amewaomba wananchi hususani wavuvi kushirikiana na Polisi na vyombo vingine vya usalama kuwatafuta watu wengine watano ambao hawajapatikana.
Sanjari na hayo amemtaka mmiliki wa mtumbwi uliopata ajali Sebastian Balakoa na nahodha wa mtumbwi huo aliyefahamika kwa jina moja la Otieno kujisalimisha kwa jeshi hilo kwa ajili ya kuhojiwa kwani walitoweka baada ya ajali.
Pia, amezikumbusha mamlaka zinazohusika na usalama majini kufanya ukaguzi kwenye mtumbwi ili kujiridhisha na uimara wake na inakuwa na vifaa vya kujiokoa endapo ajali itatokea.
Vilevile kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuzingatia umuhimu wa kuvaa maboya (life jacket) wawapo katika usafiri wa majini na kuhakikisha kwamba mitumbwi yote ya ziwani inakuwa na vifaa vya kujiokoa endapo ajali ikitokea.
Sambamba na hayo, Kamanda Mutafungwa pomoja na Mkuu wa Kikosi cha Wanamaji Mkoa wa Mwanza, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Wenceslaus Muchunguzi, wametumia nafasi hiyo kutoa elimu kwa wavuvi na wananchi wengine juu ya umuhimu wa kuvaa maboya pindi wawapo kwenye usafiri wa majini.
Pamoja na kutopanda mitumbwi ambayo tayari imezidisha abiria kupita uwezo wake hivyo inasababisha kuhatarisha usalama wa maisha yao.
More Stories
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM