Na Esther Macha, Timesmajira Online,Songwe
MKULIMA wa Kata ya Ndalambo Kijiji cha Ikana Wilaya ya Momba mkoani Songwe,, Saimon Mwakyembe,amejikuta kwenye wakati mgumu baada shamba lake la hekari 6, kuteketea na moto,uliosababishwa na watu wasiojulikana waliokuwa wakitafuta panya kwa ajili ya kitoweo cha familia.
Mkulima huyo ambaye ni mjasiriamali amewaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo limetokea Septemba 2,2025,ambapo amesema alipofika shambani kwake alikuta limeteketea kwa moto,wakati huo alikuwa ameambatana na vibarua kwa ajili ya kuvuna zao la mahindi.

“Nimeshikwa na butwaa baada kukuta shamba lote limeteketea kwa moto,hakuna nilichookoa.Hapa nilipo sina la kufanya, nimechanganyikiwa nilichukua mkopo na kununua mbegu ambapo nilijua baada ya kuvuna nitalipa,nashindwa nifanye nini nahisi kufa,”amesema Mwakyembe.
Mwakyembe amesema shamba hilo lina ukubwa wa hekari sita ambalo kila mwaka hulima mahindi na kuvuna gunia 160 mpaka 180.
“Nilichuku wanawake kutoka Rukwa, Songwe kwa ajili ya kufanya kazi ya kuvuna mahindi lakini kilichotokea ni maumivu makubwa kwangu ambayo siwezi kuelezea zaidi ya kupata hasara hii kubwa,”amesema Mwakyembe.
Jenifa Ambile mkazi wa Rukwa amesema walifika Septemba 2,2025 kwa ajili ya kufanya vibarua ili wapate hela ya mtaji ili iwasaidie kuondokana na utegemezi katika familia zao hivyo hawaelewi watafanya nini.
Faustina Dule mkazi wa Isanga amesema kuwa wamekuja kufanya kazi lakini walipofika shamba lote limeungua kwa moto ambalo tayari mahindi yalikuwa yameshakoma hivyo ikabidi warudi maana walitegemea fedha watakazoopata ziwasaidia kwenye vikundi ambavyo hukutana kila wiki.
Akizungumzia tukio hilo la shamba kuteketea kwa moto, Mwenyekiti wa Kiiji cha Ikana,Jumas Kapizi amesema wameumizwa na tukio hilo kwani wawekezaji wanasaidia wananchi kupata ajira kupitia mashamba.
,”Kesho tutafanya mkutano wa hadhara kukemea wananchi wanaochoma moto mashamba,ili wachimbe wapate panya kwa tukio hili inabidi tuendelee kufanya mikutano ya hadhara ili kuonya tabia hii,”.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Kata ya Ikana Amos Kamanga,amesema watu wanaochoma moto ni wale wanaotafuta panya,hivyo wanakemea tabia hiyo,huku akionya kuwa tukio hilo liwe la mwisho kutokea kwani wanaumiza wawekezaji ambao wanatoa ajira kwa wananchi ili kuendesha maisha yao.
,Natoa onyo kwa wananchi wote wa Nakawale, Ikana,watu wengi hawajavuna mahindi tunaomba hichi kitendo kiachwe mara moja,mnawapa hasara wawekezaji,”.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama