December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waliokunywa togwa yenye ‘sumu’ watoka Hospitali

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Ruvuma

ZIKIWA zimepita siku kadhaa, wakazi zaidi ya 100 wa kijiji cha Liula kata ya Matimaila Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma wameanza kuruhusiwa baada ya kulazwa katika kituo cha kutolea huduma cha Matimila kutokana na kusadikika kunywa togwa yenye sumu.

Mbali na kuruhusiwa kutoka katika kituo hicho cha Afya, Serikali imechukua hatua kwa wataalam wake kupinga kambi katika kijiji hicho.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt. Jairy Khanga akiongozana na wataalam kutoka ofisi ya Mganga Mkuu na Hospitali ya wilaya Songea wamefika katika kijiji hicho kwa lengo la kutoa elimu ya Afya, kudhibiti kuenea kwa madhara pamoja na kutoa majibu ya vipimo vilivyochukuliwa kwa ajili ya kutambua aina ya sumu iliyowekwa katika kinywaji hicho.

Akiongea na wakazi wa kijiji hicho mara baada ya wataalam wa Afya umaliza zoezi la kutoa dawa ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo, Dkt Khanga amesema, tukio hilo halihusiana na imani potofu za kishirikina bali maandalizi ya uandaaji wa togwa hayakuzingatia kanuni za usafi na ndiyo chanzo cha kupata maradhi yanayofahamika kwa kitaalam ‘Bacillary Dysentry’.

Dkt Khanga amesema, ugonjwa wa kuhara na kuharisha damu mara nyingi husababishwa na bakteria anayefahamika kwa jina la Shigella ambaye utokea katika maeneo yenye ukosefu wa maji safi na salama, watu wasiokuwa vyoo bora, wasionawa mikono kwa sabuni mara wanapotoka kujisaidia na kundaa chakula katika mazingira bila kuzingatia usafi.

Kwa mujibu wa Dkt Khanga, mtu (watu) wanapokosa vyoo au kujisaidia porini, kinyesi huzalisha Inzi ambao uingia katika chakula na vyombo na kuacha uchafu ambao ni hatari kwa afya ya binadamu.

Ametaja dalili za kuharisha damu ni mtu kupata homa inayoambatana na baridi kali, maumivu ya kichwa, kutapika, kuharisha na kichwa kuuma ambapo madhara yake ni kuishiwa maji mwilini na kama mgonjwa hatapata dawa ni rahisi kupoteza maisha.

Aidha, amewapongeza wahudumu wa Afya wa Zahanati ya Matimila na Liula kwa kazi kubwa waliyoifanya kuokoa maisha ya wananchi kwani mara baada ya kutokea mlipuko huo walifanya kazi usiku na mchana bila kuchoka.

Hata hivyo, amewataka wananchi kuhakikisha wanakuwa na vyoo bora na kuzingatia kanuni bora za Afya ili kuepuka magonjwa mbalimbali ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu na kuharisha.

Awali Mganga Mkuu wa Wilaya ya Songea, Dkt. Geofrey Kihaule alisema, jumla ya watu 102 walipata ugonjwa wa kichwa na kuhara damu ambapo hadi sasa hakuna aliyepoteza maisha.

Dkt Kihaule amesema, kazi iliyofanyika mara baada ya kufika katika kijiji hicho ni kutoa elimu ya afya ili wananchi waelewe namna ya kuchukua hatua pale milipuko inavyotokea na kuwaondoa hofu kuhusiana na tukio hilo na Imani ya kishirikina na kuwafuatilia wale walio karibu na wagonjwa ili nao kufahamu afya zao na kuwapa kinga ili wasipate maradhi hayo.

Baadhi ya wananchi wameipongeza Serikali kupitia Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuchukua hatua ya haraka kukabiliana na mlipuko huo hali iliyosaidia kuokoa maisha ya watu walioathirika na ugonjwa huo.

Mmoja wa wananchi hao, Moses Luambano amesema, kama wataalam wangechelewa kufika kwa wakati ni dhahiri kuwa madhara yangekuwa makubwa zaidi kwa watu kupoteza maisha.