Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Kongwa
MKUU wa Wilaya ya Kongwa Mayeka Simon amewataka wanafunzi waliofeli mtihani wa darasa la Saba mwaka 2023 kinyume na matarajio kurudia darasa hilo ili kutimiza azma ya Serikali ya Kuifanya elimu ya kidato cha nne kuwa ya lazima.
Mayeka ametoa agizo leo Januari 08, 2024, Katika ukumbi wa Shule ya Msingi Mkoka wakati akizungumza na wazazi na walezi wa wahitimu wa darasa la saba mwaka 2023 waliofeli mitihani kinyume na matarajio yanayotokana na tathmini endelevu iliyofanywa na Divisheni ya elimu ya awali na msingi.
Katika hotuba yake amesema ni suala la aibu kupoteza muda kujadili suala la wazazi kuwa kikwazo kwa watoto wao kupata elimu katika ulimwengu wa Sasa na ameahidi kuishughulikia changamoto hiyo kikamilifu.
“Kwa muda ambao Mh.Rais ataniacha Kongwa, hili halitajitokeza,”amesema Mayeka.
Hata hivyo ameipongeza Halmashauri kwa ya Wilaya ya Kongwa kwa kuweka utaratibu maalumu wa kuwasaidia wanafunzi wasio na uwezo kwa kuwalipia gharama za masomo katika ngazi mbalimbali za kielimu kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vikuu.
Aidha Mayeka ameagiza wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kuhakikisha wanakwenda shuleni hata kama hawana sare za shule, na wazazi Kila mmoja ahakikishe anatoa ushirikiano wakutosha, ikiwa ni pamoja na kupeleka chakula kwani Kwa imani yake anaamini kuwa Siri kubwa ya ufaulu wa mwanafunzi ni kupata chakula awapo shuleni.
“Hakuna kitu chochote kinachosaidia ufaulu kwa wanafunzi zaidi ya wanafunzi kupata chakula Shuleni,ema Mhe. Mayeka.
Mayeka amesisitiza wazazi kuhakikisha watoto wao wanakwenda shuleni mapema iwezekanavyo yaani siku ya Jumanne ya tarehe 09 Januari, 2024 ili kuendelea na masomo ya darasa la saba, kwani hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayepuuza agizo hilo.
Sambamba na agizo hilo amewahimiza wazazi wote wenye wanafunzi shuleni kushirikiana na walimu kuboresha zoezi la ufundishaji na ujifunzaji kwa kuhakikisha wanafunzi hao wanapata chakula wawapo shuleni kwani inasaidia kuinua kiwango cha Ufaulu. ” “Hakuna kitu chochote kinachosaidia ufaulu kwa wanafunzi zaidi ya wanafunzi kupata chakula Shuleni” alisema Mhe. Mayeka.
Ili kukomesha tabia ya watoto kuajiriwa kazi za ndani katika miji mbalimbali,Mayeka alitoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano kuwafichua madalali wote wanaojihusisha na kushawishi watoto wenye umri wa kuwa shuleni kwenda kufanya kazi za ndani.
Katika kikao hicho Wataalamu ngazi ya Wilaya, kata na vijiji wakiwemo Walimu, walichangimawazo yao, kubwa zaidi wakiahidi kushirikiana na wazazi katika jitihada za kuondoa changamoto hiyo ya aibu ya kujifelisha kwa wanafunzi.
Kufuatia hali hiyo, Mayeka amewaagiza watendaji wa Kata zote kuwasaka wanafunzi wote waliojifelisha watafutwe popote walipo ili waweze kurejea shuleni na kuendelea na masomo ya darasa la saba.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ,White Zuberi amepongeza agizo hilo ambalo limetokana na maazimio ya vikao vya kisheria vya Halmashauri na kwamba uamuzi huo unalenga kuwakomboa wanafunzi hao na kwamba wasijihisi unyonge kwa kuwa dhamira ya uamuzi huo wa kuwarejesha shuleni ni kuwakomboa na siyo kuwaumiza
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Mkuu wa Divisheni ya Elimu Awali na Msingi Mwalimu Margareth Temu amesema jumla ya Wanafunzi 416 wa darasa la saba walifeli mtihani wa taifa wa darasa la saba mwaka Jana (2023) kinyume na matarajio ingawa halmashauri ya Kongwa inajivunia kupanda ufaulu kwa asilimia 8% ikilinganishwa na matokeo ya mwaka juzi.
Ambapo amesema kati ya idadi hiyo wanafunzi wapatao 74, wanatokea tarafa ya Zoissa, 53 walishiriki kikao hicho muhimu.
Akizungumza kwa masikitiko, Spika mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Kongwa Job Ndugai amekemea tabia mbaya ya baadhi ya wazazi kuwashawishi watoto wao kujifelisha kwa malengo ya kuajiriwa kazi za ndani na kuwataka kuacha mara Moja kwani kitendo hicho hakina faida yoyote.
Ndugai amewataka watoto hao kujitambua na kufahamu kwamba maisha yao ya baadaye yanategemea sana elimu yao hivyo wanao wajibu wa kushirikiana na wazazi wao kufanikisha ndoto zao, ikiwa ni pamoja na kushiriki kwenye shughuli za uzalishaji mali ili kujikimu katika familia.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu