January 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waliojifanya Usalama wa Taifa watiwa mbaroni

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

JESHI la Polisi Mkoani Mwanza linawashikilia watu wawili waliokuwa wakijitambulisha kwa watu mbalimbali kuwa wao ni watumishi wa Serikali Idara ya Usalama wa Taifa Kitengo cha Ofisa Kipenyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ACP. Muliro Jumanne amesema, wawili hao walitiwa mbaroni Desemba 5 saa 11 jioni katika maeneo ya Kamanga Wilaya ya Sengerema .

Watuhumiwa hao ni Severine Edward Mayunga mwenye umri wa miaka 32 mkazi wa Kishiri ambaye amekutwa na kitambulisho kilichoandikwa “Severine Edward Mayunga Jamuhuri ya Muumgano wa Tanzania Idara ya Usalama wa Taifa kitengo cha kikosi maalumu code MT 82863, nafasi ya under cover na Abel Shiwa Mboja mwenye umri wa miaka 46, mkazi wa Kishiri.

Baada ya kufanyiwa mahojiano ya kina, watuhumiwa hao wamekiri kuhusika na makosa ya kitapeli na kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu hivyo watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.

Hata hivyo Jeshi hilo limetoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa zinazohusu wahalifu na uhalifu ili zifanyiwe kazi kwa haraka na watuhumiwa waweze kukamatwa kabla hawajatenda makosa.