December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waliofariki ajali ya Singida, miili yao yawasili Mwanza

Judith Ferdinand na Daudi Magesa,Timesmajira,Online, Mwanza

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella ameongoza wananchi wa Kata ya Mabatini na Jiji la Mwanza kuaga miili ya tisa kati ya 14 ya watu waliofariki kwa ajali ya basi ndogo aina ya Hiace iliyogonganana lori mkoani Singida Desemba 13, mwaka huu.

Ibada ya kuaga miili ya watu hao ilifanyika jana eneo la Kabengwe Mtaa wa Nyerere B Kata ya Mabatini Wilaya ya Nyamagana, mkoani Mwanza ambapo jumla ya miili 9 ya marehemu imeagwa.

Mongella amesema tukio hilo linasikitisha kwani watu 14 walipoteza maisha kwa pamoja.

Majeneza yenye miili ya matu tisa kati ya 16 waliopata ajali ya gari mkoani Singida Desemba 13, mwaka huu yakiagwa baada ya kuagwa jijini Mwanza eneo la Kabengwe Mtaa wa Nyerere B Kata ya Mabatini Wilaya ya Nyamagana.

“Tumepokea kwa masikitiko msiba huu,tunamuomba Mungu tuweze kuvuka jambo hili na tujikite katika ibada na tuwaombee ndugu zetu, kwani walikuwa ni sehemu ya jamii yetu na tuendelee kushikamana na familia za waliopoteza ndugu zao pamoja na sisi sote tushikamane katika kipindi hiki kigumu kwa kumuomba Mungu,” amesema.

Kati ya marehemu hao mmoja atasafirishwa kwenda mkoani Kagera na mwingine wilayani Magu kwa ajili ya mazishi.

Sheikh wa Wilaya ya Nyamagana, Athuman Ndaki,akiongoza ibada hiyo amesihi wananchi kuwa na ubinadamu na wanatakiwa kuishi kwa tahadhari kwa kuwa muungwana kwa kufuata yale yote yanayoelekezwa katika dini zao.

Kwa upande wake ndugu na rafiki wa marehemu, Rehema Hussein,Aisha Mtumwa walisema katika safari yao waliondoka watu 14, miongoni mwa walioondoka 12 waliopoteza maisha wakiwemo wanaume 6 na wanawake 6 na mtoto mchanga wa kiume.

Mtumwa alisema ajali ilitokea Mkoa wa Singida, walipopata taarifa walifuatilia miili ya marehemu hao na wanamshukuru Mungu waliweza kufika na miili hiyo saa 7 usiku wa kuamkia jana ambapo taratibu zamazishi zimeendelea.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyabulogoya, Christine Lwamba alipokuwa anasoma marehemu, Zakia Ibrahim, alisema wamepokea kwa masikitiko makubwa msiba huo wa mwanafunzi wao pamoja na ndugu wengine.

Amesema marehemu alikua na ndoto katika maisha yake na alikua amemaliza kufanya mitihani yake ya mwisho ya kidato cha tatu, hivyo mwakani angeingia kidato cha nne.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt.Phillis Nyimbi, amesema ni siku ya makubwa kwa kuaga miili 9 kati ya 12 na wamepoteza wananchi na wapendwa wao hawana jinsi kwa sababu ni ratiba ya Mwenyezi Mungu.