Na Allan Ntana,Timesmajira Online,Nzega
WALIMU 342 wa somo la kiingereza wa shule za msingi wilayani Nzega mkoani Tabora wamepewa mafunzo maalumu yanayolenga kuboresha ufundishaji wa somo hilo kwa watoto wa darasa la kwanza.
Akizungumza na Timesmajira Online Mratibu wa mafunzo hayo,Joshua Kitiko,amesema mafunzo hayo ni muhimu na yatawezesha walimu wanaofundisha somo hilo kuwa mahiri zaidi darasani.

Amebainisha kuwa mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na kampuni ya Jolly Futures ya nchini Uingereza ili kuwapa mbinu bora walimu za kuwafundishia watoto.
Amesema,walimu wa shule za msingi zote 171 za serikali zilizoko katika wilaya hiyo wanaofundisha somo la kiingereza kwa darasa la kwanza na walimu wakuu wa shule hizo ndio wameshiriki katika mafunzo hayo.
Huku washiriki wengine ni Waratibu Elimu Kata na Wasimamizi wa Elimu katika halmashauri zote 23 zilizoko katika mikoa 4, itakayonufaika na programu hiyo ambayo ni Tabora, Iringa, Arusha na Rukwa .
Mshiriki wa mafunzo hayo Stella Silutongwe ambaye ni Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Uhemeli wilayani humo, amekiri kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwani yatawapa mbinu mpya ya kufundisha somo hilo katika mtaala mpya.
Aidha ameongeza kuwa mbinu walizofundishwa zitafanya walimu wengi wapende kufundisha somo hilo na watoto wa shule za msingi za serikali sasa wataelewa kiingereza mapema tofauti na hali ilivyokuwa huko nyuma.

Mwalimu Caster Kapinga wa shule ya msingi Budushi ameeleza kuwa mafunzo hayo ni mazuri kwa kuwa yanawaandaa kufundisha somo hilo kwa weledi ili kuongeza uelewa kwa watoto kuanzia darasa la kwanza.
Mafunzo hayo yatawapa walimu mbinu bora za kufundisha somo hilo kupitia stadi za kusoma, kuandika na kutamka walizofundishwa na wataalamu wa Jolly Phonics kutoka nchini Uingereza.

More Stories
NEC yachagua wajumbe wa kamati kuu,yumo Asas
Waziri Aweso atoa maelekezo kwa Wakurugenzi huduma za maji nchini
Serikali yataka kuongezwa kwa vituo vya TEHAMA