January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Walimu S/ Sekondari Ilala wafundwa juu ya maadili ya wanafunzi

Na Agnes Alcardo, Timesmajiraonline

WAKUU wa Shule za Sekondari zilizopo katika Wilaya ya Ilala, wametakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano na weredi ili kuwepo na mwenendo mzuri kitaaluma na ufaulu katika masomo kwa wanafunzi ikiwa pamoja na maadili.

Akifungua mafunzo kwa walimu wakuu wa Shule za Sekondari za Serikali na binafsi, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, leo Jijini Dar es Salaam, kwenye mkutano wa mafunzo kwa walimu hao ukihusisha na Ma- Afisa Watendaji Kata 36 za Wilaya ya Ilala na wadau wa elimu.

Amesema ni vyema kila Mwalimu akatambua wajibu wake katika kuhakikisha anatoa elimu bora kwa wanafunzi na kusema kuwa, kufanya hivyo kutasaidia kuendelea kutokomeza ziro katika shule mbalimbali na kuwaandaa watendaji na viongozi bora wa baadae katika Taifa.

Mpogolo amesema, Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kiasi kikubwa imeboresha mazingira ya utoaji elimu, hususani katika miundombinu ya madarasa na ongezeko la vifaa vya kufundishia.

Amesema, katika Wilaya ya Ilala, Wilaya hiyo ilipatiwa Sh. bilioni 35 kwa upande wa Elimu Sekondari, ambapo kazi kubwa iliyofanyika ni pamoja na ujenzi wa shule za kisasa za ghorofa.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wakuu hao wa shule, kuonesha ushirikiano kwa walimu wa ngazi za chini katika masuala mbalimbali yanayosaidia kuinua taaluma na si kuwatenga na kuwanyima nafasi ya kuhudhuria au kutoa maoni hususani katika vikao muhimu.

“Wapeni nafasi kwa sababu mafanikio ya shule yanachangiwa na walimu hao lakini sifa mnapata ninyi wakuu wa shule, Ofisa Elimu, Mkurugenzi wa Halmashauri na mimi Mkuu wa Wilaya na sifa zote hizo ni kutokana na wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao, lakini ukiangalia hadi mwanafunzi amefanya vizuri sababu ni kule chini ambapo ni mwalimu aliyemfundisha darasani,” amesema Mpogolo.

Pia, Mpogolo amewasisitizia walimu hao juu ya kuheshimiana wao kwa wao na viongozi wa Halmashauri bila ya kufahamiana zaidi, akisema kuwa, kufanya hivyo ni kutimiza na kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora bila ya mipaka.

“Kuna wakati mwalimu anakuwa na changamoto, anatuma ujumbe wa kuomba ruhusa, mkuu wa shule unausoma halafu hujibu, au mwalimu anamtumia ujumbe Ofisa Utumishi naye anausoma lakini hajibu hii haifai na inaonesha kuwa hakuna mahusiano mazuri ”amesisitiza Mpogolo.

Sambamba na hayo, Mpogolo amesisitiza juu ya usimamizi na ulinzi wa kutosha kwa wanafunzi ili kuepusha kuwepo na wanafunzi wasiyo na sifa nzuri za kinidhamu.

Pamoja na hilo, Mpogolo aliwataka walimu kusaidia kusimamia maadili ya wanafunzi kwani wapo wanafunzi watukutuku wanao tembea na visu, mikasi, mawe, viwembe na bisbisi katika mabegi yao hivyo kutishia usalama.

“Walimu tujitahidi kusimamia maadili ya wanafunzi wetu wawapo shuleni, kwani wapo wanafunzi Wana tabia zisizofaa na asizostahiri kuwa nazo mwanafunzi kwani wapo wanafunzi wanaotembea na visu, mikasi, viwembe nk hii haifai walimu tuwajibike katika hili na ikiwezekana tutumie hata polisi kata kuwapekua wanafunzi hawa.

Nyie walimu ndiyo mnakaa na watoto kwa kipindi kirefu kuliko mzazi na kuna wazazi wanaogopa kuwaeleza ukweli watoto wao hivyo tusaidie kulinda maadili ya watoto hawa,”amesema Mpogolo.