Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Chamwino
SHIRIKA la kusaidia watoto wanaopita kwenye changamoto mbalimbali (CIC) limeanza kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu wa elimu ya awali katika mradi wa Watoto WetuTunu Yetu katika Wilaya za Kongwa na Chamwino mkoani Dodoma.
Mafunzo hayo ya siku nne yameshirikisha pia Walimu Wakuu, Waratibu wa Elimu kata na Maafisa Elimu Kata kutoka Wilaya hizo ili kujenga nguvu ya pamoja katika utekelezaji wa mradi huo.
Akitoa utangulizi wa mafunzo hayo katika utekelezaji wa mradi huo, Mkufunzi kutoka CiC Frank Samson amesema mradi huo ni wa miaka mitatu ambao utatekelezwa katika shule 58 za Wilaya ya Kongwa na Chamwino.
Katika mradi huo yatatengenezwa madarasa ya awali ya mfano lengo likiwa ni kufikia shule za msingi 700 zilizopo katika Mkoa wa Dodoma ifikapo mwaka 2022. Shirika hilo linaangazia malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
Mradi huo ambao umeanza miaka minne iliyopita unatekelezwa na CiC kwa kushirikina na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais Tamisemi na tayari umetekelezwa katika mikoa ya Mwanza na Morogoro, ambayo imefanya vizuri katika utekelezaji wake.
“Mwanza na Morogoro wamefanya vizuri na Dodoma mfanye vizuri katika kata zenu na CiC itafuatilia karibu ili kufikia malengo ya mradi huo.
Kwa upande wake Mdhibiti Mkuu Ubora wa Elimu Wilaya ya Chamwino, John Balisidya amewataka walimu washiriki wote kuyachukulia mafunzo hayo kwa umuhimu mkubwa ili kufanikisha mradi huo.
Afisa kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Idara ya Usajili wa Shule, Musa Mapunda amesema, mradi huo ni wa muda mrefu ambao unatarajiwa kutoa matokeo chanya kupitia walimu.
Kwa upande wake Msimamizi wa Elimu ya Awali kutoka Tamisemi, Salvatory Alute amesema stadi wanazopata katika mafunzo hayo zikatumike hususan katika kipindi hiki ambacho watoto wa awali wamepoteza kila walichokuwa wameanza kufundishwa kabla ya shule kufungwa kutoka na janga la ugonjwa wa Corona.
“Kwa sasa watoto ni kama wanapokelewa upya, walikuwa hawajazoea shule bado, lakini sasa walimu mnapewa mbinu nyingine muwe tayari kuwarudisha watoto darasani haraka,” amesema Alute
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi