November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Walimu Bunda wapongezwa matokeo ya kidato cha sita

Na Raphael Okello, Timesmajira Online,Bunda.

KATIBU Tawala wa Wilaya ya Bunda , Salum Mtelela amewapongeza watumishi wote wa shule ya sekondari Bunda,wilayani humo mkoani Mara kwa kuwezesha shule kushika hiyo kushika nafasi ya kwanza kimkoa na 19 kitaifa katika matokeo ya kidato cha sita mwaka huu.

Mtelela amesema hayo katika hafla mahususi ya kutambua jitihada za watumishi hao walizofanya katika kuwafundisha wanafunzi na kufanya vizuri katika mtihani wa kidato cha sita kwa miaka mitatu mifululizo.

Katibu Tawala amewataka walimu kuendeleza nguvu na juhudi ili wazidi kufanya vizuri zaidi na kuendelea kuitangaza Halmashauri ya Mji wa Bunda na Wilaya ya Bunda kwa ujumla.

Aidha, Katibu Tawala ametoa ahadi ya zawadi toka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kiasi cha 490,000 sambamba na kuwapeleka katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kama watalii wa ndani.

Awali Mkuu wa shule ya sekondari Bunda, Charles Somba ameeleza mafanikio makubwa ambayo shule imeweza kuyapata kwa takribani miaka mitatu mfululizo.

Amesema kwa mwaka 2021 jumla ya wanafunzi waliofanya mtihami walikuwa 88 kati yao 73 walipata daraja la kwanza na 15 walipata daraja la pili shule ilishika nafasi ya pili kimkoa na 21 Kitaifa.

Mwaka 2022 waliofanya mtihani walikuwa 115 kati yao waliopata daraja la kwanza ni 104, wanafunzi 10 daraja la pili na mmoja pekee alipata daraja la 3 ambayo shule hiyo ilishika namba mbili kimkoa na nafasi ya 15 Kitaifa.

Somba amesema kwa mwaka huu 2023 wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa 126 kati yao wanafunzi 121 walipata daraja la kwanza, wanafunzi 4 walipata daraja la pili na mwanafunzi mmoja pekee alipata daraja la tatu na kwamba shule imefanikiwa kushika nafasi ya kwanza kimkoa na 19 Kitaifa.

Mwalimu Somba aliwashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza kuwapongeza ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, wadau wa elimu akiwemo Alphayo Kidata, Juma Makongoro.

Somba alipongeza pia Kanisa la AICT Dayosis ya Mara na Ukerewe Kwa kusaida shule hiyo kupata maji Kwa kuchimba kisima cha maji chenye thamani ya milioni 30.