January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Walengwa wa TASAF washauri kuwa na matumizi mazuri ya fedha

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Wanufaika wa mradi wa Kunusuru Kaya Maskini Tanzania (TASAF), wilayani Ilemela mkoani hapa wameshauriwa kuwa na mpango na matumizi mazuri ya fedha wanazozipata ili kupunguza makali ya maisha na kumudu mahitaji yao ya msingi.

Wito huo umetolewa na Ofisa Ufuatiliaji mradi wa TASAF Wilaya ya Ilemela Alex Kabona wakati akizungumza na baadhi ya walengwa katika mitaa mbalimbali kwa nyakati tofauti ambapo amesema ni wajibu wa walengwa na watu wa karibu yao kuwashauri vema kufanya matumizi sahihi ya fedha wanazopewa ili kuleta nafuu katika kumudu mahitaji yao ya msingi.

Ambapo ameeleza kuwa anafahamu kuwa miongoni mwao wameanzisha vikundi vya kuchanga fedha na kukopeshana ni jambo zuri.

“Tunahitaji mbadilike matumizi mabovu kama kulewa pombe hayana nafasi hapa,mnapokea fedha hakikisheni mnaweka akiba angalau kwa uchache kwa kuwa mpo wengi mnapigana tafu kwa baadae mnaeza kujadili pamoja vitu vya kufanya zaidi kutokana na makusanyo,”amesema Kabona.

Kwa upande wake mmoja wa walengwa wa TASAF mkazi wa Nyasaka Center ambaye ni mjane Stella Makoye ameeleza kuwa ana watoto sita wote wapo shuleni ambapo ana unafuu mkubwa kwenye kuwahudumia watoto wake akisaidiwa na mradi wa ufugaji kuku aliouanzisha mwaka jana tangu alipoingia kwenye mpango huo wa TASAF.

“ Nashukuru serikali kupitia mradi huu watoto wangu kwa sasa wana uhakika wa kupata milo mitatu na kupata mahitaji yao yote madogo madogo ya msingi,Mungu awabariki sana muendelee kutuona mara kwa mara kama hivi.”

Zoezi la uhawilishaji fedha linaendelea ambapo jumla ya kiasi cha millioni 534.6 kwa ajili ya awamu mbili za malipo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 zinaendelea kutolewa kwa kaya 5868 za walengwa ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.