November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Walengwa wa TASAF Korogwe TC waendelea kunufaika

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe

KAYA 2,602 za wanufaika wa Mpango wa kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga, wameendelea kuneemeka baada ya kulipwa milioni 125.5.

Katika malipo hayo, kaya 1,636 zimelipwa sh. milioni 84 kwa njia ya simu (mtandao) na kaya 966 zimelipwa milioni 41.5 kwa fedha taslimu.

Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wakiwa Ofisi ya Mtendaji Mtaa wa Old Korogwe wakisubiri malipo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Aprili 3,2024 Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Mji Korogwe Rehema Letara amesema malipo hayo ni ya Novemba na Desemba 2023.

Letara ambaye amechukua nafasi ya aliyekuwa Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Mji Korogwe tangu kuanzishwa kwake, Goodluck Kiboma, amesema atashirikiana na jamii kuona wanafanikisha miradi yote iliyopangwa kutekelezwa kwenye halmashauri hiyo.

Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa wakiwa Ofisi ya Mtendaji Mtaa wa Kwasemangube, Kata ya Magunga wakisubiri malipo.

“Nimejipanga kushirikiana na watumishi wenzangu pamoja na wananchi kuona tunasimamia miradi yote inayotekelezwa na jamii,najua kuna changamoto za mara kwa mara kutoka kwa baadhi ya walengwa, ikitokea basi tunamwita mhusika ofisini na kuchukua taarifa zake, kisha na sisi tunazituma TASAF Makao Makuu ili kupatiwa ufumbuzi,” amesema Letara.