Na Waandishi Wetu, TimesMajiraOnline, Morogoro
WAKUU wa Vitengo vya Mawasiliano vya Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha, wametakiwa kuendelea kutangaza majukumu yanayofanywa na taasisi zao kikamilifu ili kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu miradi ama kazi zinazotekelezwa na Taasisi hizo na kuchangia kukuza uchumi na maendeleo ya nchi.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Jenifa Omolo, wakati akifungua Kongamano la Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano na Masoko vya Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo pamoja na Wahariri wa Vyombo vya Habari lililofanyika katika Ukumbi wa 8-8, mkoani Morogoro.
Amewasisitiza Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano wote kutumia jukwaa hilo kujadili na kubadilishana uzoefu wa masuala mbalimbali ya Mawasiliano ya Umma na usambazaji wa taarifa kwa wadau, na kujadili changamoto zinazowakabili ili kuzipatia ufumbuzi utakaoongeza ufanisi katika utendaji kazi na utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kwa maendeleo yao na ustawi wa Taifa kwa ujumla.
Omolo amefafanua kuwa Mawasiliano ndio msingi wa mafanikio wa kila jambo, na kupitia mawasiliano Taarifa njema zinazohusu Taasisi zinaweza kusomwa na wadau mbalimbali wa ndani na nje na kuelewa mambo mazuri wanayoyatekeleza, hivyo wana wajibu wa kuhakikisha kuwa wanazingatia Mawasiliano imara ya kimkakati ili kujenga Taswira chanya kwa Wizara, Taasisi na Taifa kwa ujumla.
Amesema kuwa lengo kuu la kongamano hilo lilikuwa kujadili na kubadilishana uzoefu wa masuala mbalimbali ya Mawasiliano ya Umma na usambazaji wa taarifa kwa wadau zinazohusu Wizara na Taasisi zake.
“Nimefarijika sana kuona kwamba mmeitikia wito wa kushiriki katika Kongamano hili, hii ni ishara njema kwa ustawi wa Wizara na Taasisi zake katika kukuza na kuimarisha Mawasiliano kwa Umma. Ni matumaini yangu kuwa siku za usoni kongamano hili litakuwa ni miongoni mwa makongamano bora na makubwa zaidi nchini” amesema Omolo.
Awali, akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Jenifa Christian Omolo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Benny Mwaipaja, amewapongeza wahariri na vyombo vya habari nchini kwa namna zinavyosukuma agenda ya Maendeleo na kutangaza habari zinazochagiza ukuaji wa uchumi wa nchi na kuifanya Tanzania iwe kinara katika Usimamizi na ukuaji wa uchumi katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.
Amesema kuwa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, limesifu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kusimamia uchumi na Vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuhakikisha kuwa nchi inasimamia sera zake za uchumi na fedha kwa umahili
Naye Mwenyekiti wa wahariri wa vyombo vya habari wa Kongamano hilo, Ben Mwang’onda, ameshukuru Wizara ya Fedha kwa kuandaa kongamano hilo ambalo limekuwa daraja la mahusiano kati ya Wizara hiyo na Umma katika kutoa taarifa mbalimbali.
Hilo ni Kongamano la pili la Mawasiliano kufanyika kati ya Wizara ya Fedha na Taasisi zilizo chini yake ambazo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Soko la Bidhaa Tanzania-TMX, Chuo cha Uhasibu Arusha-IAA, Mfuko wa Self-SELF Microfinance, Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini – IRDP, Mamlaka ya Rufaa ya Zabuni za Umma – PPAA, Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini – GPSA, Mfuko wa Uwekezaji – UTT-AMIS, Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi – PSPTB, Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Ununuzi wa Umma – PPRA, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania – TIRA, Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika – EASTC, Benki ya Maendeleo ya Kilimo – TADB, Hazina Saccos na Shirika la Bima la Taifa – NIC.
More Stories
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Maandalizi ya mkutano mkuu CCM yapamba moto