November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakurugenzi watakiwa kusimamia upandishaji madaraja ya walimu kwa wakati

Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara.

SERIKALI Mkoani Mara imewataka Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri zote za Wilaya Mkoani humo kusimamia kwa ufanisi wakati zoezi la upandishaji wa madaraja kwa waalimu pamoja na maslahi yao.

Kauli hiyo imetolewa Oktoba 4, 2024, na Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka wakati wa maadhimisho ya siku ya Mwalimu yaliyofanyika Uwanja wa Karume Manispaa ya Musoma.

Kupitia hotuba yake Kanali Mtambi amesema kuwa Serikali inatambua na kuthamini kwa dhati mchango na juhudi zinazofanywa na Walimu Mkoani humo katika kusimamia msingi wa malezi ya watoto kitaaluma na kusimamia maadili yao.

“Ni wajibu wetu Viongozi kusimamia haki zenu na maslahi yenu kwa ufanisi, niwatake Wakurugenzi wote wa Halmashauri simamieni vyema na kwa wakati kuhakikisha Walimu wanaopaswa kupanda madaraja wapande kwa wakati ,jambo hili msipolifanya likafika ofisini kwangu nitachukua hatua.Lazima Serikali tuendelee kuwaangalia kwa macho mawili kusimamia stahiki na haki zenu.”amesema Kanali Mtambi.

Pia, Kanali Mtambi amewataka Waalimu kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi kwa kufundisha Watoto kwa bidii, moyo wa upendo na kuhakikisha dhamana waliyopewa inazidi kuongeza tija.

Aidha Mtambi amesema serikali ya Awamu ya Tano imefanya ukarabati wa shule mbalimbali Kongwe Mkoani humo pamoja kuendelea kujenga shule mpya ili Watoto wapate elimu bora,hivyo Wazazi na walezi wanalojukumu la kudumisha ushirikiano na Walimu na kufuatilia maendeleo yao ya Watoto wao kitaaluma.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini Vedastus Mathayo amesema kuwa, ataendelea kuchukua changamoto zote za Walimu na kuzifikisha serikakili ili kuleta ufanisi wa majukumu yao.

Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi iliyoandaliwa na Kamati ya Utendaji ya Chama cha Walimu Tanzania ( CWT) Manispaa ya Musoma, Mwalimu Edward Kunyara amesema Walimu katika Manispaa hiyo wapo tayari kulinda hadhi yao na kuhakikisha vituo wanavyofanyia kazi vinakuwa vitovu vya hazina ya maandiko kwa maisha ya Watanzania wa leo na kesho.

“Kwa pamoja tunatambua na kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wake kwa Walimu nchini ikiwemo upandishaji mishahara na madaraja kwa Walimu hasa kima Cha chini cha Mshahara katika kipindi chake cha uongozi.”amesema Mwalimu Kunyala.

Pia, ongezeko la asilimia 7, la mafao kwa Walimu wastaafu kutoka asilimia 33, hadi kufikia 40. Na ujenzi wa miundombinu bora masshuleni na vitendeakazi kwa Walimu.

Ametaja changamoto zinazowakabili Walimu wa Manispaa hiyo katika utekelezaji wa majukumu yao kuwa ni pamoja na ucheleweshwaji wa madaraja kwa Walimu, kutopata ongezeko la mshahara kwa kila mwaka kisheria hali inayopelekea Walimu kuwa na hali ngumu ya kimaisha kulingana na soko la mahitaji ya kila siku na mfumuko wa bei za bidhaa.

Changamoto zingine ni ufinyu wa bajeti kutotosheleza malipo ya stahiki za Walimu likizo na masomo ya Walimu pamoja na Kilio cha Wastaafu kutumika kwa kanuni ya 580 badala ya 540 kwenye kikokotoo. Hivyo kuchangia Wastaafu kuishi maisha duni na ya mashaka kwa kutokuwa na uhakika wa kuishi kwa fedha ya kichele.

Siku ya Mwalimu duniani iliasisiwa na UNESCO kila tarehe 5, ya mwezi oktoba kila mwaka. Ambapo Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Walimu katika kiini cha kupona kwa elimu”. Ambapo katika Manispaa ya Musoma Walimu wameshiriki michezo mbalimbali.