Na Moses Ng’wat, Momba.
WAKURUGENZI wa Halmashauri Mkoa wa Songwe wametakiwa kuhakikisha kuwa wanatenga bajeti ya kutosha na kusimamia mipango ya utekelezaji wa shughuli za Elimu ya watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo rasmi (EWW na ENMR).
Agizo hilo limetolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Momba, Elias Mwandobo, wakati wa kilele cha madhimisho ya juma la elimu ya watu wazima yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Ndalambo,Wilaya ya momba.
“Serikali imendelea kutekeleza program zingine za EWW/ENMR katika mkoa wetu kwa lengo la kumwinua mwanasongwe, hivyo ni wajibu kwa wakurugenzi kuhakikisha mnatenga bajeti ya kutosha na kusimamia mipango ya utekelezaji wa shughuli za Elimu ya watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo rasmi,” amesema Chongolo.
Kupitia hotuba yake hiyo, Chongolo amewataka Wakurugenzi Watendaji hao pia, kuhakikisha wanaendelea kutekeleza ipasavyo mpango wa Shule Salama za msingi na sekondari unatekelezwa katika shule zote za mkoa ili kuimarisha mahudhurio na ubora wa elimu shuleni
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka, watendaji hao, Kusimamia ujenzi wa miundombinu yote ya shule ambayo inaletewa fedha na serikali pamoja na ile inayojengwa kwa nguvu za wananchi pamoja na fedha za mapato ya ndani.
Vile vile, amewataka watendaji hao wa Halmashauri kuwatumia wanafunzi wa IPOSA na vikundi mbalimbali vya MUKEJA katika kazi na miradi mbalimbali ili kuinua vipato vyao, hasa katika ujenzi, utunzaji wa mazingira, upimaji wa ardhi na kuwasaidia kusajili vikundi ili wapate mikopo.
Pia katika hotuba hiyo, Chongolo amewataka wakurugenzi hao kuhakikisha shule zote za kutwa zinatoa chakula lishe cha mchana na kuhakikisha shule za bweni zote wanafunzi wanapata chakula lishe.
Awali Ofisa elimu Mkoa wa Songwe, Majuto Njanga, amesema katika kutekeleza program mbalimbali za elimu, Mkoa huo umefanikiwa Kuwarudisha shuleni wanafunzi 211 wa kike wa sekondari waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito.
More Stories
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu