Na Martha Fatael, TimesMajira Online, Moshi
SERIKALI imetaka wakulima wa mazao ya aina mbalimbali kutumia ripoti za wataalamu wa Kilimo ili kulima mazao kulingana na Afya ya Udongo kuliko Kilimo Cha sasa kisicho na tija.
Kwa sasa wizara ya Kilimo inafanya utafiti kubaini Afya ya Udongo katika baadhi ya halmashauri nchini, ikiwamo wilaya ya Moshi ili kuwashauri wakulima kufuata utaalamu huo ili kulima kisasa zaidi.
Kaimu mkurugenzi idara ya mipango na maendeleo Bora ya Ardhi kutoka wizara ya Kilimo, Mhandisi Juma Mdeke, kwenye mafunzo ya wakulima na wataalam wa ugani katika wilaya ya Moshi vijijini kuhusu umuhimu wa kupima Afya ya Udongo kabla kuanza Kilimo.
Amesema ili kufikiwa kwa lengo hilo, wizara ya Kilimo inaandaa muongozo kwa wakulima katika mikoa mbalimbali nchini ili kutambua aina ya mazao wanayopaswa kulimwa katika maeneo yao.
“Asilimia kubwa ya ardhi yetu ina Magadi na Tindikali inayoathiri mazao….lipo tatizo la wakulima wetu wanalima tu kwa kutumia uzoefu badala ya utaalamu tunataka mabadiliko katika hili” anasema.
Amesema wizara itatoa muongozo kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya chokaa kwa ajili ya kutibu Udongo usiathiri mazao yatakayolimwa.
Naye ofisa Kilimo, umwagiliaji na ushirika wa Halmashauri ya wilaya ya Moshi, Fidoline Mpanda amesema Maeneo ya ukanda wa juu wa wilaya hiyo kuna Tindikali na Magadi ambavyo ni adui wa Kilimo.
Amesema wizara kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya inafanya utafiti katika maeneo ya ukanda wa juu wa wilaya hiyo ili kujua Afya ya udongo kabla ya kuwashauri wakulima.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti