November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

OLYMPUS DIGITAL CAMERA

Wakulima watakiwa kujikita kwenye kilimo cha kisasa

Na Angela Mazula,TimesMajira Online

MFUKO wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) umewataka wakulima nchini kujikita katika kilimo cha kisasa kinachoendana na ukuaji wa sayansi na teknolojia kwa lengo la kukabilina na umasikini kwenye maeneo yao.

Akizungumzia hilo, mwakilishi wa IFAD Jackiline Motcho amesema, ipo haja ya wakulima kuongeza wigo wa uzalishaji hatua ambayo itawasaidia kukabiliana na janga la njaa katika maeneo mbalimbali duniani.

Amesema, Mfuko huo umekuwa ukishirikiana na Serikali ya Tanzania kwa kuanzisha miradi ya kutoa hamasa kwa wakulima wadogo kujikita katika kilimo cha kisasa, badala ya kuendelea na kilimo cha mazoea ambacho wengi wamekuwa wakilima kwa ajili ya chakula pekee, hali ambayo hukwamisha ukuaji wa sekta hiyo muhimu.

“Tumefanya na Serikali kuanzia mwaka 1978, kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa chakula, wakulima kulima kilimo chenye tija zaidi tumewekeza katika mnyororo wa thamani ili kufungua milango ya masoko kuanzia shambani hadi soko la ndani na nje ya nchi na siyo kilimo tu, pia tunasimamia sekta ya ufugaji na uvuvi Tanzania Bara na Visiwani,” amesema Mwakilishi huyo.

Motcho amewataka wakulima kutumia fursa ya miradi ambayo imekuwa ikianzishwa na IFAD itakayowasaidia kuongeza ujuzi na uelewa katika masuala ya kilimo, huku akiwasisitiza kushiriki katika semina zinazojitokeza ili kupata uzoefu kutoka kwa wakulima wabobezi na kupata changamoto, akisema kwamba kilimo kikitiliwa mkazo kinaweza kuleta mageuzi ya kimaendeleo.

“Miradi yetu yote tunafanya na hili kundi la wakulima wadogo na kuna mradi wa MIVARF utakaomalizika Desemba, tulikuwa tunaangalia mkulima tangu uzalishaji hadi kuongeza thamani ‘market access’ lengo apate ahueni na kuona manufaa ya kazi ya mikono yake”, amesema Motcho.

Hata hivyo aliwahimiza maofisa ugani kushirikiana na wakulima kuwapa elimu ya kilimo bora, kwani ni sekta inayohitaji elimu ya mara kwa mara kutokana na kubadilika kwa njia za uzalishaji, kuwashauri kilimo kinachofaa kulingana na mazingira husika na mabadiliko ya hali ya hewa.

“Nitoe wito kwa maofisa kilimo kuketi meza moja na wakulima kuwapa elimu ya kilimo cha kibiashara tusiwaache peke yao tunatakiwa tuvuke pamoja kama tunavyofahamu kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa,” amehimiza Mwakilishi huyo.

Hata hivyo, ameitaka jamii kubadili fikra juu ya sekta ya kilimo kuona kwamba hufanywa na watu wa hali ya chini akisema mtu yeyote anaweza kufanikiwa kupitia kilimo, hivyo ni lazima kuwa na nguvu ya pamoja kwani kupitia mazao kumewezesha uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata bidhaa mbalimbali hatua inayochagiza pato la mtu mmoja mmoja naTaifa kwa ujumla.

“Baadhi ya watu huona kama wakulima ni watu walioshindwa maisha lakini niwaambie wakulima hawa ni watu muhimu sana katika maisha ya kila siku maana shambani ndiko chakula kinapozalishwa na tunategemea tule ili tuishi ni wakati sasa wa kubadili fikra zetu wapo mabilionea wengi wamefanikiwa kupitia kilimo,” amesema Motcho.

%%%%%%%%%%%%%%