Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online Mbeya
BAADHI ya wakulima wa parachichi mkoani Njombe wameiomba Serikali kuweka miundombinu wezeshi kwenye Bandari ya Tanga ikiwemo umeme wa kutosha ili kuweza kupoza mazao yao yasiharibike kabla ya kusafirishwa kwenda masoko nje ya nchi.
Pia wametaka Serikali kuweka chumba cha baridi (Cold room) kwenye mikoa ya Mwanza, Dodoma, Tanga na Dar es Salaam ili kuhifadhi mazao ya mbogamboga na matunda kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
Hayo yamesemwa Agousti Mosi, 2023 na Mkulima Bora wa Parachichi Mkoa wa Njombe Frank Msuya alipokuwa anamueleza Mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa kuhusu mafanikio na changamoto zinazowakabili wakulima wa parachichi.
Ambapo kauli hiyo ametoa katika banda la Halmashauri ya Mji Njombe katika maonesho ya Nane Nane Kimataifa yanayofanyika mkoani Mbeya.
Msuya ambaye ni Mwenyekiti wa Havila Farm iliopo Kijiji cha Nundu, Kata ya Yakobi, Halmashauri ya Mji Njombe mkoani Njombe, alimueleza Mkuu wa Wilaya hiyo Kasongwa kuwa zao la parachichi lina soko kubwa nje ya nchi, hivyo kama Serikali itawasaidia kuondoa changamoto zinazowakabili, wataweza kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa ikiwemo kupata fedha za kigeni.
“Sisi wakulima wa parachichi tunaiomba Serikali, Bandari ya Tanga ndiyo itumike kusafirisha mazao yetu ya mbogamboga na matunda ili iweze kusafirisha mazao haya ni lazima iwe na umeme wa kutosha ili yale magari yanayosafirisha mazao yetu ambayo tayari yana cold room, yatumie umeme wa TANESCO wakati yakisubiri kupakia bidhaa kwenye meli badala ya kutumia umeme wa gari,”amesema na kuongeza kuwa
“Kwenye mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam na Dodoma kuwe na cold room ili kuhifadhi mazao ya mbogamboga na matunda kabla ya kusafirishwa kupelekwa bandarini,itasaidia mazao ya wakulima yanayotoka Arusha, Kilimanjaro na Tanga, au parachichi kutoka Mbeya, Njombe na Iringa kubaki na ubora wake hadi yatakapofika sokoni,”.
Msuya amesema pia wanataka Serikali iondoe urasimu njiani hasa kuhusu mazao ya mbogamboga, na kutolewe kibali ambacho kitaruhusu mzigo kukaguliwa mara mojo na njia nzima kitaonesha mazao hayo yamekaguliwa, badala ya kila kwenye kizuizi mazao hayo kukaguliwa kwa kupekuliwa, na hivyo kuyatoa baridi iliyopo, huku yakicheleweshwa njiani.
“Tunaomba Serikali itoe Green Pass (kibali cha mazao ya kilimo) ili kuwaondolea usumbufu watu wanaosafirisha mazao hayo wakiwa njiani,utakuta njia nzima kuna vizuizi hadi 10,wengine wanataka kufungua cold room, hivyo kufanya baridi kupungua, huku wakichelewesha mzigo kupelekwa kwa wakati sokoni,tunataka kama mzigo umekaguliwa unapotoka, basi gari lisisimamishwe tena njiani,”amesema Msuya.
Msuya ambaye ana shamba la ekari 150 za parachichi, huku ekari 30 zipo tayari kuvunwa, anatumia milioni 20 kwa msimu mmoja (miezi saba) kwa ajili ya kusukuma maji kwenda kwenye mashamba ya parachichi, hivyo Serikali iwawekee umeme ili maji ya visima virefu wanayovuta kwa jenereta, waweze kuvuta kwa kutumia umeme.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Kissa Kasongwa, alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Kuruthum Sadick, kwani amewezesha kutoa dawa za kuua wadudu bure kwa mazao mbalimbali ikiwemo parachichi, hivyo zao hilo la parachichi kuwa na ubora.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa