Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya OCP Tanzania imetumia Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane yanayoendelea jijini Mbeya kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi ya mbolea ya Triple Super Phosphate (TSP) – 00-46-00, mbolea ya kupandia yenye kiwango kikubwa cha fosforasi inayosaidia ukuaji wa mizizi na ustawi wa mazao katika hatua za awali.
Kupitia ushirikiano na wakulima, wauzaji wa pembejeo na wadau wa sekta ya kilimo, OCP Tanzania imekuwa ikifafanua umuhimu wa lishe ya awali kwa mazao ili kuongeza mavuno na kustahimili changamoto za mazingira. Kampuni hiyo pia imesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha TSP inapatikana kwa bei nafuu ili kuwafikia wakulima wa ngazi zote.
Akizungumza hatua hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere, alipongeza mchango wa OCP Africa, amesema jitihada za kampuni hii zinaendana na malengo ya serikali ya kuhakikisha usalama wa chakula na kuendeleza kilimo endelevu.

Wakulima waliotembelea banda la OCP wamepatiwa mafunzo ya vitendo kuhusu matumizi ya TSP katika mazao kama mahindi, mpunga, mikunde na viazi. Meneja Masoko wa OCP Africa Tanzania, Zaward Green Hankungwe, alisema: “Kilimo chenye uhakika huanza na TSP. Tukitumia virutubisho sahihi tangu kupanda, afya ya mazao huimarika na tija ya soko huongezeka.”

Nae, Mariam Mwakalukwa, mkulima kutoka Chunya, amesema mafunzo hayo yamemsaidia kupata uelewa wa kuongeza mavuno bila kuongeza gharama kubwa.
Maonesho ya Nane Nane Mbeya yanaendelea kuwa jukwaa la ubunifu na ushirikiano, likiwaunganisha wadau wa sekta ya kilimo katika mnyororo wa thamani, huku OCP Africa ikiendelea kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea za kupandia kama TSP kwa mafanikio ya kilimo nchini.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi