December 1, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima waishukuru CRDB

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Mbeya

BAADHI ya wakulima mkoani Mbeya wameishukuru benki ya CRDB mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa imewasaidia kupata mikopo ya fedha na nyenzo ikiwemo trekta aina ya Power Tiller ambavyo vitawainua kwenye kilimo na kipato.

Ambapo wakulima zaidi ya 600 kutoka Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wanatarajiwa kupatiwa mkopo na CRDB wa zana za kilimo ikiwemo trekta, power tiller, zana za kuvunia, fedha za mikopo ya kulimia na pembejeo za kilimo ikiwemo mbegu, mbolea na dawa pamoja na mikopo ya stakabadhi ghalani.

Mkuu wa Kitengo cha Kilimo Biashara wa CRDB Maregesi Shaaban (kulia) akitoa maelezo mbele ya Rais Dkt. Samia, alipotembelea banda la benki hiyo kwenye maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) yanayofanyika kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Mmoja wa wakulima hao kutoka Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya Halima Ally, alitoa ushuhuda huo Agosti 8, 2023 mbele ya Rais Dkt. Samia alipotembelea banda la CRDB kwenye maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) yaliyofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

“Sisi wakulima wa Mbarali tunaishukuru CRDB kwa kutuwezesha kupata mikopo ya fedha na zana za kufanyia kazi kama ilivyotukopesha power tiller hii ambayo itaniwezesha kuendeleza kilimo changu cha mpunga na mahindi,” amesema Ally.

Rais Dkt. Samia, aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuweza kukopesha wakulima kwa riba ya asilimia tisa, huku akiitaka benki hiyo kuendelea kufuatilia zana za kilimo wanazowakopesha wakulima ili ziendelee kufanya kazi,ikibidi kuwasaidia kutengeneza pindi zinapoharibika, kwani baadhi yao zana hizo zikiharibika, wanazitelekeza.

“Nawapongeza CRDB kwa kuweza kutoa mikopo yenye riba ya asilimia tisa,itawasaidia wakulima kuweza kukopa kwa wingi na kulima kwa tija,mikopo ya power tiller mnayotoa kwa wakulima muifuatlia na kuwasaidie waweze kutengeneza kwani wakati mwingine power tiller linaharibika na kulitelekeza hivyo kushindwa kuleta tija,”amesema Dkt. Samia.

Baadhi ya wananchi wakipata huduma katika banda la CRDB katika maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) yanayofanyika kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Awali, Mkuu wa Kitengo cha Kilimo Biashara wa CRDB Maregesi Shaaban amesema benki hiyo imeendelea kutoa mikopo inayofikia trilioni 3.9 kwa misimu mitano iliyopita hadi kufikia Julai, 2023, sawa na asilimia 43 ya mikopo yote itolewayo na benki kwenye sekta ya kilimo na mifugo nchini.

Amesema wanatoa mafunzo kwenye vituo atamizi chini ya mpango maalum wa BBT kupitia Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi,wanaendelea kutoa elimu ya fedha na usimamizi wa miradi kwenye vituo vilivyoko nchini,uwezeshaji vijana na wanawake kwenye kilimo, uvuvi, mifugo, viwanda na biashara Bara na Visiwani.

“Benki kupitia kampuni yetu tanzu ya CRDB Bank Foundation, inawekeza kwa vijana na wanawake ili waweze kutimiza ndoto zao ikiwa ni pamoja na kuwapa mafunzo na kuwapatia mitaji kwa ajili ya uanzishaji wa miradi mipya (startup capital),ambayo hutolewa kwa vijana na wanawake wenye mawazo bunifu kibiashara na benki inatoa mitaji ya awali ikiwa ni mbegu itakayoleta matunda na kuwafungulia kesho yao yenye tija zaidi kiuchumi, chini ya program ya kipekee ijulikanayo kama IMBEJU,”amesema Shaaban.

Shaaban amesema benki hiyo imefanikiwa kufufua matumaini ya wana ushirika kwa kuongezea mtaji inayofikia bilioni 10.2, ambapo bilioni 3.2 kwa TACOBA na bilioni 7.0 kwa KCBL.

Ambapo awali taasisi hizo zilikuwa zikijiendesha kwa hasara na baada ya kupata mtaji na usimamizi madhubuti kutoka CRDB, zimeanza kujiendesha kwa faida kubwa na kutokana na mikakati madhubuti ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia, wanaendelea kutekeleza ndoto nzuri ya kiuchumi ya uanzishwaji wa Benki ya Ushirika ya Taifa.

Baadhi ya wananchi wakiingia kwenye banda la CRDB ili kupata huduma mbalimbali katika maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) yanayofanyika kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Shaaban amesema,benki hiyo ikishirikiana na wauzaji wa vifaa madhubuti vya kilimo (Agricom), imeweza kuwakabidhi baadhi ya wanufaika waliopata mikopo ya kununua power tillers kwa ajili ya kilimo cha mpunga mkoani Mbeya.

“CRDB itaendelea kushirikiana na Serikali ya ili kuendeleza fursa za uwekezaji zilizopo Bara na Visiwani,”.

Baadhi ya wananchi wakipata huduma katika banda la CRDB katika maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) yanayofanyika kwenye Viwanja vya John Mwakanga jijini Mbeya.