Na Jackline Martin, TimesMajira Online
BENKI ya Equity imetia saini mkataba wa ushirikiano wa kibiashara (MoU) na taasisi isiyo ya kiserikali-Movement for Community Development (MCODE) pamoja na PASS TRUST lengo ikiwa ni kuwafikia wakulima wadogo wadogo zaidi ya 200,000 ambao wapo vijijini na wanahitaji kupata huduma za kifedha hususani mikopo.
Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mkataba huo, Meneja Mkuu wa Biashara – Benki ya Equity, Leah Ayoub, alisema mbali na kuwapa mikopo hiyo wakulima, pia wanawapa mafunzo jinsi ya kutumia kwa usahihi mikopo wanayowapa.
“Benki ya Equity inaamini kupitia uwezeshaji wa wakulima wadogo wadogo walio katika vikundi kutaiwezesha benki kufikisha huduma za kifedha kwa wananchi wengi zaidi, hivyo kutimiza adhima ya Serikali ya kuboresha sekta ya kilimo ambayo imeajiri watu wengi na yenye mchango mkubwa zaidi katika pato la taifa.
Ni dhamira ya Benki ya Equity kufanya kazi na wadau wote wenye malengo na maono yanayoendana na Serikali katika kuhakikisha inachangia juhudi za Serikali kwenye sekta ya kilimo hasa hasa Agenda 2030. “Alisema
Pia alisema wataendelea kutoa mikopo yenye gharama nafuu ambayo haitamuumiza mkulima ambayo itamfanya mkulima huyo akishamaliza kuvuna ataweza kulipa mkopo na kubaki na faida.
“Lengo letu hasa kama Equity ni kuboresha maisha ya mtanzania, mkulima mdogo hadi aweze kuwa mkulika mkubwa ambaye anaweza akajitegemea akawa na trekta lake pia akaweza kuchakata yake mazao ambayo anayavuna”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa PASS TRUST, Adam Kamanda, alisema ubia huo umeongeza wigo wa kufanya kazi zaidi hata kwa kutoka kwenye zao la mahindi na kwenda kwenye mazao mengine katika nchi mbalimbali.
Pia wataendelea kuhakikisha idadi hiyo ya wakulima inaongezeka zaidi hadi kufikia watu 100,000.
“Tunaishukuru sana Benki ya Equity, ubia huo utaendelea kudumu, tutafanya kazi sana tukitembea na kuongeza tija kwa wakulima katika mnyororo mzima wa mazao katika sekta nzima ya kilimo, mifugo na Uvuvi”
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya MCODE, Slaiton Kaberege alisema awali walikuwa wakifanya kazi kwenye mazao ya mahindi pekee hivyo wanaendelea kuongeza nguvu kwenye kaimu unaoisha na unaofata kwenye mpunga, viazi na parachichi kutokana na mkoa husika.
Hadi sasa tayari wakulima wadogo wadogo zaidi ya 30,000 wa zao la mahindi katika mikoa ya Ruvuma, Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe na Rukwa wamefikiwa kwa kupewa mikopo yenye thamani ya sh. Bilioni 20.
More Stories
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo