January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima wa tumbaku walivyoongeza uzalishaji miaka mitatu ya Rais Samia

Na Jumbe Ismailly,Timesmajiraonline

SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwaandalia mazingira mazuri na thabiti wakulima kwa kupitia vyama vya msingi vya ushirika vya mazao ya kilimo na masoko (Amcos) ili viweze kuwa na uwezo wa kuzalisha mazao ya kilimo na biashara.

Vyama hivyo vya mazao ya kilimo na masoko vimekuwa vikizalisha mazao ya kimkakati kama vile pamba, kahawa, korosho,chai pamoja na tumbaku ambavyo kwa muda mrefu sasa wakulima wa mazao hayo hawakuwa wakinufaika kutokana na kuwepo kwa mifumo holela ya ununuzi.

Kibaya zaidi mfanyabiashar aalikuwa akinunua mazao hayo kwa kutumia vipimo kama vile kangomba, kibubu, butula, kadumula, rumbesa, choma choma na magoma vilivyokuwa vikimdidimiza mkulima.

Njia pekee ambayo imekuwa mkombozi kwa mkulima ambaye ndiye mvuja jasho ni kujiunga pamoja na kuimarisha pamoja nguvu zao kupitia vyama vya ushirika vya msingi, ambavyo katika miaka ya hivi karibuni vilikuwa vimekosa nguvu kutokana na uwepo wa wafanyabiashara ambao walikuwa wakipita vijijini kununua mazao kwa bei ya chini.

Katika kuelekea siku ya kupinga matumizi ya tumbaku duniani, inayotarajiwa kuadhimishwa Mei 31, mwaka huu wakulima wa zao la tumbaku wa Chama cha Ushirika cha Msingi Manyanya (Manyanya Amcos) kilichopo Kata ya Mitundu, Halmashauri ya Itigi, Wilaya ya Manyoni, Mkoani Singida wamechangishana fedha na kujenga ghala la kuhifadhia mazao ili kukabiliana na uuzaji wa mazao kwa bei ya chini ukilinganisha na gharama walizotumia.

Hata hivyo wakati wakulima wa zao la tumbaku wa Manyanya Amcos wakichukua maamuzi magumu ya kuchangishana fedha na kisha kujenga ghala la kuhifadhia mazao ili kukabiliana na uuzaji wa mazao kwa bei ya chini,Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni (WHO) limezitaka nchi zinazotoa ruzuku kwa wakulima wa tumbaku kuacha mara moja kutoa ruzuku hiyo kwa wakulima wa tumbaku na badala yake waelekeze nguvu zao kuwasaidia wakulima kwenye mazao endelevu yatakayo wanufaisha mamilioni ya watu.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa hivi karibuni Nchini Geneva Uswisi,WHO inasema kwamba kwa kuchagua kulima mazao ya chakula badala ya tumbaku inamaanisha jamii inatoa kipaumbele kwenye afya,kulinda bainowai pamoja na kuimarisha uhakika wa chakula.

Mkurugenzi mkuu wa WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus akizungumzia athari za tumbaku anasema kuwa tumbaku imesababisha vifo vya zaidi ya watu milioni nane kwa mwaka na bado serikali duniani kote zinatumia mamilioni ya fedha kuwasaidia wakulima wa zao hilo.

Hata hivyo ripoti mpya iliyotolewa na WHO kuelekea siku ya kupinga matumizi ya tumbaku iitwayo “Lima chakula sio tumbaku”imeeleza madhara ya kulima tumbaku na faida ambazo wakulima,jamii,uchumi,mazingira na dunia kwa ujumla itapata iwapo itahamia kwenye ukulima wa mazao mengine.

Mwenyekiti wa CEAMCU LTD, Daudi Amosi Ngayaula(wa tatu kutoka kushoto) akimsikiliza Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Singida, Nipeneema Mfuru(wa nne kutoka kushoto) alipokuwa akimuelezea umuhimu na faida za ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao mbali mbali kabla ya kuweka jiwe la msingi la jengo la ghala la chama cha Manyanya Amcos.

Aidha ripoti hiyo pia inafichua tasnia ya tumbaku kuwa inawaingizia wakulima katika changamoto mbalimbali ikiwemo mzunguko mbaya wa madeni,wakulima kupata magonjwa na watoto zaidi ya milioni moja kutumbukia kwenye kilimo hicho na kukosa fursa ya kupata elimu.

Katika siku ya kupinga matumizi ya tumbaku duniani iliyoadhimishwa Mei,31, mwaka uliopita,WHO inasema jumla ya watu milioni 300 ulimwenguni wanakabiliwa na uhaba wa chakula wakati huo huo zaidi ya hekta milioni tatu katika nchi 120 zinatumika kulima tumbaku,hususani katika nchi zile zenye tatizo la njaa.

Katika kuelekea siku ya kupinga matumizi ya tumbaku duniani,inayotarajiwa kuadhimishwa Mei 31,mwaka huu wakulima wa zao la tumbaku wa Chama cha Ushirika cha Msingi Manyanya (Manyanya Amcos) kilichopo Kata ya Mitundu, Halmashauri ya Itigi,Wilaya ya Manyoni,Mkoani Singida wamechangishana fedha na kujenga ghala la kuhifadhia mazao ili kukabiliana na uuzaji wa mazao kwa bei ya chini ukilinganisha na gharama walizotumia.

Hata hivyo katika msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023 wakulima wa zao la tumbaku wa Wilaya ya Manyoni, Mkoani Singida walinufaika na kilimo cha zao hilo kwa kupata jumla ya shilingi bilioni tisa na milioni mia saba kupitia vyama vya ushirika baada ya kuzalisha kilogramu milioni mbili na laki moja za tumbaku kwa msimu huo.

Aidha katika uzinduzi wa soko la tumbaku kwenye msimuwa kilimo wa mwaka 2022/2023 uliofanyika kata ya Mitundu,Halmashauri ya Itigi,wilayani Manyoni wakulima wa zao hilo walizungumzia fursa ya kilimo hicho kwa kuwa miaka kadhaa iliyopita kilimo hicho kilionekana kusuasua kutokana na kukosekana kwa masoko.

Kutokana na ongezeko la bei,vyama vya ushirika vilinufaika na kutoa hamasa kwa wakulima kuendelea kulima ziada katika msimu huu kama anavyoeleza katibu meneja wa chama cha ushirika cha msingi Manyanya,Iddi Yaredi Mlewa kwenye hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao mbali mbali likiwemo zao la tumbaku.

Kwa mujibu wa Mlewa katika msimu wa miaka mitatu kuanzia msimu wa mwaka wa 2021/2022 uzalishaji wa zao la tumbaku ulikuwa kilo 509,374.97 hadi msimu wa mwaka 2023/2024 ambapo katika msimu wa mwaka 2021/2022 chama hicho kilizalisha kilo 82,900,000 wakati kilo 176,474.97 zilizalishwa mwaka 2022/2023 na kwa mwaka 2023/2024 zilizalishwa kilo 250,000.

Katibu meneja huyo anaweka wazi malengo ya ujenzi wa ghala hilo kuwa ni kutatua changamoto ya kukodi ghala la kuuzia tumbaku kwa misimu iliyopita na ndipo mkutano mkuu maalumu wa wanachama uliofanyika septemba,15,mwaka 2023 waliazimia kuchanga kila mwanachama shilingi 738,000/=kwa ajili ya ujenzi wa ghala hilo.

Akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la ghala la kuhifadhia tumbaku,Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Singida,Nipaneema Mfuru anasema Mkoa wa Singida umedhamiria kwa dhati kupunguza umaskini wa kipato kwa wananchi wake kwa kupitia shughuli za kijamii na kiuchumi.

Anasema Nipaneema kuwa katika kilimo mkoa umekuwa ukihimiza wananchi kulima mazao ya chakula na biashara yanayoendana na hali ya hewa ya Mkoa wa Singida na kwa kufanya hivyo wananchi wataweza kuwa na chakula cha kutosha na hali kadhalika kuuza mazao ya biashara na kujipatia fedha kwa matumizi mbali mbali.

Hata hivyo mrajisi msaidizi huyo anasema katika uuzaji wa mazao yao,wananchi wamekuwa wakikumbana na changamoto mbali mbali hasa uuzaji wa mazao kama vile pamba,alizeti,tumbaku, dengu,ufuta,choroko pamoja na korosho kwa bei ya chini ukilinganisha na gharama walizotumia,ukosefu wa soko la kuaminika la mazao mbali mbali yanayolimwa katika Mkoa wa Singida.

Mrajisi msaidizi Mkoa wa Singida,NIPENEEMA MFURU(wa tatu kutoka kulia) akikata utepe kushiria kuweka jiwe la msingi la jengo la ghala la kuhifadhia mazao ya wakulima wa tumbaku wa Manyanya Amcos,kilichopo Kata ya Mitundu,Halmashauri ya Itigi wilayani Manyoni,Mkoani Singida.(Picha zote Na Jumbe Ismailly)

Mrajisi msaidizi huyo anabainisha kuwa zao la tumbaku na pamba hununuliwa kupitia vyama vya msingi (AMCOS) huku mazao mengine hununuliwa na wanunuzi binafsi kupitia mfumo usio rasmi wa nyumba kwa nyumba,hali ambayo hupelekea wakulima kuuza mazao yao kwa bei yeyote ile anayotaka mnunuzi.

Nipaneema anazitaja faida za ujenzi wa ghala hilo kuwa ni pamoja na kuwapa wakulima nguvu ya soko kwa kupitia ukusanyaji wa mazao pamoja kwenye ghala,kuwa na sehemu salama ya kuhifadhia mazao,kufanya ushirika uzidi kuimarika kwa kuongeza ushirikiano na wadau mbali mbali wanaofanya kazi na vyama vya ushirika, kuimarisha biashara na soko la mazao kwa kuongeza ufanisi katika ubora wa mazao na kuimarisha mfumo wa ukusanyaji,uchambuzi na usambazaji wa taarifa na takwimu na kuongeza thamani ya mazao na kuwezesha ushirika kujiendesha kibiashara kikiwa kama kipaumbele kimojawapo katika vyama vyetu vya ushirika.

Fortunatha Tadei aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Magefa Growers Ltd ambayo ni kampuni ya kwanza na kampuni ya wadada anasema kitendo kilichooneshwa na wanachama wa chama cha msingi kinawapa matumaini kwa asilimia mia moja kwamba Kampuni hiyo ina uhakika wa kupata mzigo wa tumbaku bila shaka yeyote.

Anasema Fourtunata pia kuwa kupitia chama cha msingi Manyanya anaviomba vyama vingine ambavyo vina changamoto kama Manyanya viige utamaduni huo mzuri na kwamba ni imani ya kampuni hiyo kwamba kila chama kitakuwa na maghala kwa utaratibu kama uliotumiwa na Manyanya Amcos.

Mkulima wa zao la tumbaku Abrahamu Mika Mongo anasema awali hawakuwa na mahali pa uhakika pa kuuzia tumbaku kutokana na kutokuwa na ghala na hivyo kulazimika kukodi maghala na hatimaye kupata bei mbaya,lakini kwa awamu hii wana uhakika wa kuuza mazao yao kwa uhakika na kwa bei nzuri.