November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima wa kahawa wapewa mbinu kukabiliana na konokono

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

TAASISI ya Utafiti wa Kahawa Tanzania(TacRi) imesema katika msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2024 zao hilo limepata changamoto ya wadudu waharibifu aina ya konokono ambao hufanya uharibifu hata kwa mazao mengine na kusababisha hasara ya uzalishaji kwa wakulima.

Wizara ya Kilimo imefanya jitihada kwa watalaam kupita Mkoa mzima wa Songwe na Mbeya katika kata ambazo zilikuwa zimepata mashambalizi ya wadudu hao na kutoa elimu pamoja na mbinu mbalimbali zinazofaa katika kukabiliana na konokono.

Kauli hiyo imetolewa Agosti 3,2024 na Meneja wa Kanda za Juu Kusini (TacRI) Dismas Pangalas kwenye maonesho ya Nanenane yanayofanyika uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya ambapo maonesho hayo yanafanyika kikanda.

Hata hivyo Meneja huyo amefafanua kuwa kiwango cha athari katika thamthimini za awali imeonekana kuwa mashambalizi ya wadudu aina ya konokono yanaweza kusababisha kupoteza miche ya kahawa kwasababu ya kufa kwa asilimia 2 mpaka 3.

Pangalas amesema inaonesha kuwa kasi ya kuzaliana kwa Konokono ni kubwa inaweza kuleta athari kwa siku za mbeleni.

Hivyo watafiti na wadau kutoka Bodi ya Kahawa wameshirikiana kutoa elimu kwenye vyama vya msingi 24, kwa mikoa miwili ambayo ni Songwe na Mbeya ili wakulima kufahamu mbinu za kukabiliana na konokono.

“Natoa Rai kwa wakulima kuwa katika kipindi hichi cha mabadiliko ya tabia nchi hususani ambacho kumetokea ongozeko la magonjwa na wadudu ambao walikuwa hawapewi kipaumbele ni vema kuwa na tahadhari,”amesema.

Pia amesema wamekuja na Teknolojia ya kutumia mtegoe kuwanasa Konokono kwa kutumia kitunguu swaumu na asali na ili kuweza kuwahi wadudu hao kabla ya kufikia uharibifu na kuwapunguza idadi yao.

Kwa upande wake Mtafiti na Mkurugenzi wa TacRI ,Charles Mwingira amesema kuwa pamoja na kufanya utafiti wamekuwa wakiweka mkazo maalum katika usambazaji wa teknolojia ili kuhakikisha matokeo ya utafiti yanawafikia wakulima kwa haraka.

“Tunazo aina bora za kahawa ambazo zinatolewa na taasisi yetu hazishambuliwi na magonjwa makuu ya zao la kahawa ikiwemo ugonjwa wa kutu ya majani pia aina hizo za mbegu zinazaa vizuri,”amesema Mwingira.

Mwingira amesema kuwa katika miaka ya hivi karibuni kuna mdudu anaitwa Luhuka amekuwa akisumbua zao la kahawa ingawa sio sana kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini,jitihada za kutoa elimu bado zinaendelea kwa wakulima ili waweze kukabiliana na mdudu huyo .

Amesema mdudu huyo anakula kahawa ikishaiva kwani ikianza kuiva inakuwa na radha ya pombe ambayo inamvutia mdudu huyo na kuwa katika tafiti zao wamegundua kuweka mitego na kumnasa kwa kuweka kilevi huku mwanzoni katika hatua za awali walikuwa wakitumia spiriti kuthibiti mdudu huyo .

“Tumejaribu pia kutumia pombe za kienyeji mfano ,kimpumu,mbege,ndengelua,lubisi, na ulanzi pl kuthibiti mdudu huyu unajua kahawa ni kinywaji na sehemu kubwa tunauza nje ya nchi,”amesema .

Mmoja wa wakulima kutoka Songwe ,Bryson Nzunda amesema kuwa wadudu hao wamekuwa changamoto kwao hasa msimu wa mvua ambapo wadudu hao huwa wengi .

“Elimu inayotolewa na watalaam tumekuwa tukipokea na kuifanyia kazi katika kuthibiti wadudu hawa mfano konokono mara nyingi yeye anaonekana kipindi cha mvua kutokana na majimaji kuwa mengi hivyo ni mdudu ambaye anakuja kwa msimu lakini ni mwaribifu sana kwenye zao hili la kahawa,”.