October 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima Tabora wagoma kuuza Tumbaku

Na Allan Vicent, TimesMajira Tv, Uyui

WAKULIMA wa zao la tumbaku katika kata ya Mabama, Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora wamegoma kuendelea kuiuzia tumbaku kampuni ya Voedsel kwa madai ya kutolipwa madeni yao ya zaidi ya dola za kimarekani 120,000.

Mbali na kugoma, wakulima hao pia wanataka kuchukua tumbaku yao iliyoko katika maghala ya kampuni hiyo ambayo walishamuuzia mapema mwaka huu lakini hawajalipwa fedha zao.

Akizunguza na gazeti hili mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Chamba cha Msingi Malumba (Amcos), Jumanne Haruna amesema kuwa hawana imani na kampuni hiyo, ndiyo maana wanashinikiza awalipe fedha zao la sivyo watachukua tumbaku yao yote.

Ameeleza kuwa wanadai kutolipwa fedha zao za soko la kwanza lililofanyika Mei 15 mwaka huu ili waweze kuendelea na masoko mengine na kampuni hiyo la sivyo hawako tayari kuendelea kuiuzia tumbaku yao.

‘Hadi sasa kampuni hii haijatulipa fedha zetu za awali tofauti na makubaliano, ndiyo maana tunashinikiza watulipe kwanza ili kuendelea kuwapa mzigo mwingine, huo ndiyo utaratibu wa masoko ya tumbaku’, amebainisha.

Aidha Mwenyekiti ameomba serikali kupitia Bodi ya Tumbaku (TTB) kuingilia kati sakata hilo ili waweze kulipwa fedha zao zote ambazo ni zaidi ya dola za kimarekani 120,000 na asipowalipa achukuliwe hatua za kisheria.

Wajumbe wa Bodi ya Chama hicho, Emmanuel Matandiko na Musa Yasini wamesema kuwa kwa mujibu wa kanuni za masoko ya tumbaku ukiuza tumbaku yako unatakiwa kulipwa ndani ya siku 7 hadi 14, lakini muda umeshapita.

Wamesisitiza kuwa wameipa masaa 24 kampuni hiyo ili kuhakikisha inalipa stahiki zote za wakulima wa chama hicho vinginevyo arudishe mabelo yao yote yaliyoko katika maghala yake ili waiuzie kampuni nyingine.

Licha ya Mwandishi wa gazeti hili kufanya jitihada za kuwatafuta Maafisa wa kampuni hiyo ili kutolea ufafanuzi sakata hilo, wahusika waliingia ndani ya maghala na kujifungia.

Meneja wa Bodi ya Tumbaku Kanda ya Magharibi Albert Charles amekiri kufahamu sakata hilo na kuongeza kuwa ni kweli soko hilo lilifanyika Mei 15 mwaka huu na wakulima hao hajawalipwa fedha zao.

Ameeleza kuwa baada ya Bodi kupokea malalamiko hayo na kuanza uchunguzi wa awali, walibaini kuwa Mei 15 mwaka huu wakati wa soko hilo mabelo 29 yalikuwa na tumbaku chafu hivyo yakaondolewa na kubakia mabelo 771.

Ameongeza kuwa licha ya kuondolewa mitamba hiyo kampuni hiyo ilifanya ujanja ujanja na kuichukua tena kinyemela, hivyo akaomba wakulima hao kuwa na subira wakati suala hilo likifuatiliwa ili waweze kulipwa stahiki zao.