Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Mbeya
MPANGO wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (“SAGCOT”) umeelezwa kuwa na mafanikio hapa nchini ambapo umeweza kuwafikia wakulima zaidi ya 400,000 na kuongeza uzalishaji wao wa mazao shambai kati ya wakulima milioni 2 wanaopaswa kufikiwa ifikapo mwaka 2030.
Hayo yamesemwa na Maria Ijumba kutoka SAGCOT wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la SAGCOT kwenye maonyesho ya wakulima Nane Nane jijini Mbeya .
“Mafanikio katika kufikia wakulima na ukanda huu ni makubwa sana ,kwa mfano hao wakulima 400,000 ni wale ambao tumewafikia sisi kama SAGCOT ,lakini wapo wakulima wanaofikiwa na wadau ambao wamepata utaalam kutoka kwetu kwa hiyo ukiangalia mafanikio ya kufikia wakulima idadi yake inaweza kuzidi hadi milioni 2 kiasi ambacho tumepangiwa kukifikia.”amesema Ijumba
Kwa mujibu wa Ijumba, SAGCOT inafanya kazi kuratibu maendeleo ya kilimo Nyanda za Juu Kusini ambapo wanafanya kazi kwa ubia wa serikali na sekta binfasi katika kuhakikisha uzalishaji wa mazao shambani unakuwa wenye tija.
Amesema,katika maonyesho ya mwaka huu wameleta wadau zaidi ya 30 wa sekta binafsi na wakulima wa mazao mbalimbali pamoja na wafugaji.
“Hapa katika mabanda ya SAGCOT kuna sekta nyingi katika mabanda haya,pia tunafanya kazi na serikali kuhusu masuala ya utafiti ili kupata mbegu bora zitakazowasaidia wakulima kuzalisha kwa tija,
“Kwa hiyo sekta nyingi utakuta kwenye haya mabanda ,wa mbolea,wa mbegu,utakuta utafiti tunafanya kazi na serikali katika eneo la utafiti kwa sababu ili uwe na mbegu bora unahitaji utafiti,utakuta katika mabanda yetu kuna huo mnyororo kuanzia kwenye utafiti hadi kwa anayesindika ,utakuta wakulima ambao wamenufaika na uratibu wa SAGCOT.”amesema
Kwa mujibu wa Ijumba,katika uratibu wanaofanya,wakulima wanafundisha wakulima wenzao katika matumizi ya teknolojia na kuhakikisha uzalishaji wa mazao shambani unaongezeka kwa manufaa ya mkulima mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
“Wakulima wamepeleka telnolojia ya viazi ,mpunga na parachichi kutoka Mkoa wa Njombe ,Iringa mpaka Sumbawanga,Rukwa ,Ruvuma huko kote wakulima wananfundishana wao kwa wao.”
Kwa upande wake Zeno Mgaya Mwenyekiti wa Agri Bussines inayojishughulisha na masuala ya Mkulima kwa Mkulima kwa maana ya kuchukua wakulima wazoefu na kuwapeleka eneo ambalo wakulima hawana uzoefu wa zao Fulani na kubadiliana uzoefu huku akisema wamejikita katika uzalishaji wa mazao ya parachichi na viazi mviringo.
Aidha amesema kilimo wanachofanya ni kilimo biashara ambacho kinaanzia kwenye tafiti za udongo ,mbegu bora,kutunza hadi kutunza kumbukumbu kwa maana ya lazima mkulima atunze ya kile anachokifanya ili kuonyesha anajitambua.
Vile vile Mwenyekiti huyo amesema,katika kuwafanya wakulima hao wanakuwa wamoja wamewaundia vyama vya Ushirika (AMCOS) ili kupata wadau na kufikiwa na mabenki kwa urahisi.
Hiyo pia inawawezesha kujua masoko na kuwawezesha kulima kwa tija kutokana na kujua soko linataka nini tofauti na zamani mkulima alikuwa anaanza kulima ndipo anaenda kutafuta soko.
Mkulima wa mazao mchanganyiko kutoka mkoa wa Mbeya Mistoni Mbwiga amesema maonyesho ya mwaka huu yameandaliwa vizuri na hivyo kufanya mkulima anapofika kwenye mabanda kupata maelezo kutokana na maswali anayouliza ambayo yanakwenda kumsadia katika kuongeza uzalishaji.
Utekelezaji wa SAGCOT unachukua kipindi cha miaka 20 mpaka mwaka 2030 tangu kuanzishwa kwake 2010 lengo likiwa ni kuongeza tija ya uzalishaji kwenye kilimo, kuimarisha usalama wa chakula, kupunguza umaskini na kuhakikisha uhifadhi endelevu wa mazingira kupitia urasimishaji wa kibiashara kwa wakulima wadogo.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa